Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza jambo wakati wa mkutano na wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Mkoani Mtwara, Leo 19 Januari 2018.
Wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa Mkutano wa pamoja na wachimbaji hao kwenye ofisi za Madini Kanda ya kusini, Leo 19 Januari 2018.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Kanda ya kusini Ndg Peter Ludovick akieleza kero za wachimbaji mbele ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo,
Wizara ya Madini imesisitiza wachimbaji wadogo
na wakubwa nchini kutambua umuhimu wa ulipaji kodi kwa kila wanachozalisha
kwani itasaidia kuongeza pato la Taifa kwa kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili nchi ikiwemo ukarabati wa miundombinu, Ujenzi na uimarishaji Wa
sekta ya afya, elimu, Sekta ya umeme na sekta ya maji.
Akizungumza Mkoani Mtwara wakati wa mkutano na
wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka
Biteko amesema kuwa jamii bado haina elimu ya kutosha juu ya ulipaji kodi hivyo
ofisi za madini nchini zinapaswa kuongeza msukumo Wa utoaji elimu juu ya
ulipaji kodi na utunzaji wa kumbukumbuku za shughuli za uvunaji Madini kwa kila
mahali kwenye leseni.
Mhe Biteko alisema kuwa wachimbaji wadogo kote
nchini wanapaswa kutambua kuwa hawatakiwi kusalia kukwepa kodi badala yake
wanapaswa kutoka kwenye uchuuzi na hatimaye kuhamia kwenye ufanyabiashara na
kuhifadhi taarifa zote kwa mujibu wa kanuni kwa kipindi cha miaka 5.
Alisema kuwa mtu yeyote anapoitwa
mfanyabiashara anatambulika katika jamii na serikali kwa ujumla wake hivyo
kigezo kikubwa na muhimu kwa mfanyabiashara ni kulipa kodi kwa mujibu Wa
kanuni, sheria na taratibu.
Akizungumza kwa msisitizo Mhe Biteko alisema
kuwa watanzania wamempata Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuongoza Taifa akiwa Rais
Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano hivyo
wanapaswa kuunga mkono juhudi za utendaji wake kwa kulipa kodi kwa manufaa ya
jamii nzima.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Wa Madini
ameupongeza uongozi Wa Ofisi ya Madini Kanda ya Mtwara kwa ushirikiano mzuri na
wachimbaji jambo ambalo limeimarisha utendaji wao pasina malalamiko dhidi ya
serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti Wa Chama Cha
wachimbaji Mkoa Wa Mtwara Ndg Festo Balegele akizungumza wakati Wa mkutano huo
alimsihi Naibu Waziri wa Madini kutilia mkazo uongezaji thamani wa chumvi
inayozalishwa nchini kwa kuikausha (Drying) na kuisaga (Grinding) sambamba na
kuongeza Madini joto kwani itapelekea serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni
zinazotumiwa na serikali kuagiza chumvi nje ya nchi.
Alisema kuwa kila mwaka jumla ya tani 350 za
chumvi huagizwa nje ya nchi ambapo ikiwasili nchini inauzwa kwa shilingi 500
kwa gramu 500 sawa na shilingi 50,000 kwa kilo 50 kiasi ambacho ni kikubwa Mara
tano ya gharama za chumvi inayozalishwa nchini kwani inauzwa kwa shilingi 5000
kwa kilo 50.
Alisema kuwa chumvi inayoagizwa nje ya nchi ni
kiasi cha Tani 350,000 kila mwaka huku akisisitiza kuwa serikali ingetilia
mkazo na kuboresha miundombinu nchini ingerahisisha upatikanaji wa chumvi
nyingi nchini ambayo inauzwa kwa kiasi kidogo chenye uwezo wa kukidhi mahitaji
ya watanzania.
No comments:
Post a Comment