Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Juma akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya sheria leo jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia
tarehe 27 hadi 31,Januari 2018. Kushoto ni Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand
Wambali na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Hussein Kattanga.
Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Wambali akifafanua jambo mbele ya waandishi
wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Profesa Ibrahim Juma (kulia) kuhusu maadhimisho ya wiki ya sheria leo jijini
Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Mnazi
Mmoja kuanzia tarehe 27 hadi 31, Januari 2018. Kushoto ni Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Rufaa Mhe. Catherine Revocati.
Msajili Mkuu wa Mahakama Catherine Revocati akielezea jambo mbele ya
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wao na Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Juma (wapili kutoka kulia) leo jijini Dar es Salaam.
Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga na Jaji Kiongozi Ferdinand
Wambali.
Hayo yameelezwa leo
jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma
alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maonesho ya maadhimisho ya
Wiki ya Sheria nchini yenye maudhui ya ‘Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa
wakati na kwa kuzingatia maadili’.
“Kila mwaka Mahakama ya
Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria ambayo huashiria kuanza rasmi kwa shughuli
za Mahakama, kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi na Rais
Magufuli katika viwanja vya Mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar es
Salaam,” amesema Jaji Mkuu Juma.
Jaji Mkuu amesema kuwa
kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Mahakama ya Tanzania pamoja
na wadau muhimu katika Sekta ya Sheria watatumia siku tano kuanzia tarehe 27
hadi 31 Januari mwaka huu kwa ajili ya kufanya maonesho yatakayotoa elimu kwa
wananchi watakaopata nafasi ya kuhudhuria katika viwanja vya Mnazi Mmoja
vilivyopo jijini humo.
Maonesho hayo
yatatanguliwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria yatakayofanyika
Januari, 28 mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yatakayoanzia katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Rais Mstaafu Kikwete
atazindua rasmi Wiki ya Sheria.
Aliongeza kuwa Wiki ya
Sheria inatoa nafasi nzuri kwa wananchi kuzifahamu shughuli mbalimbali
zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wa sekta ya sheria ili kufanikisha
maboresho endelevu ya Mahakama.
Aidha, Jaji Mkuu Juma
amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama itaendelea kupokea malalamiko na mawazo
kutoka kwa wananchi na kuyafanyia kazi hata baada ya Wiki ya Sheria kuisha.
Wiki hiyo ya Sheria
itaenda sambamba na uzinduzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama yaliyokamilika
yakiwemo ya Mahakama ya Mwanzo Kawe, Kituo cha kisasa cha mafunzo Kisutu pamoja
na Mahakama ya WIlaya ya Bagamoyo, Mkuranga na Kigamboni.
Wadau wengine
watakaoshiriki katika wiki ya sharia pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Mafunzo ya Uanansheria
kwa Vitendo Tanzania, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi,
na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali.
No comments:
Post a Comment