Mgodi wa dhahabu wa Geita, GGM umekabidhi mradi wa kuwawezesha vijana na
wanaweke kujikwamua kiuchumi wenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 2 kwenye
halmashauri ya mji wa Geita.
Mradi huo unahusisha shughuli za uchomeleaji wa vyuma, ushonaji wa nguo,
utengenezaji wa viatu na ufyatuaji wa matofali ya kisasa.
Hatua hiyo imefuatia uamuzi wa serikali mkoani Geita kutaka ikabidhiwe
majengo ya mradi huo yaliyojengwa kwa ufadhili wa mgodi wa GGM yaliyopo Mtaa wa
Magogo yabadilishwe kuwa Chuo cha Ufundi, VETA kwa lengo la kuwasaidia vijana
wengi zaidi kupata ujuzi wa ufundi Mkoani humo.
Akizungumza katika makabidhiano ya mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel amesema atahakikisha taratibu za kuwa chuo zinakamilika
kwa muda mfupi huku akiagiza Halmashauri ya Mji wa Geita kusimamia kikamilifu
jambo hilo.
Mmoja wa wajasiriamali walio katika mradi huo Bw Isack Mabula amesema
tangu wawekwe kwenye mradi huo hawajafanikiwa kujiendeleza kutokana na mgodi
kugoma kuendelea kuwafadhili.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Geita ametoa onyo kwa wote wanaohujumu miradi ya maendeleo
ya wananchi.
Manase Ndoroma ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa GGM amesema mategemeo yao
ni kuona mradi huo ukiendelezwa na serikali na kwamba Utawanufaisha wananchi
wengi zaidi hususani vijana na wanawake.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary
amesema mradi huo utatoa fursa nyingi za kuwawezesha walengwa kujifunza na
hatimaye kujitegemea katika shughuli za kiuchumi
No comments:
Post a Comment