Mila potofu na umbali wa vituo vya afya zimetajwa kuwa kati ya sababu za
baadhi ya wajawazito kujifungulia nyumbani wanapopatwa na uchungu katika
Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.
|
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya
cha Uyovu Wilayani Bukombe Dr Steven Kazuzu alisema uelewa wa wananchi
kuhusu kujifungulia kwenye vituo vya afya ni mdogo na kwamba wengine wamekuwa
na imani potofu kwamba Mwanamke anapojifungulia nyumbani kuna baadhi ya viungo
hubaki navyo tofauti na akijifungulia hospitalini.
“Tatizo kubwa ambalo linasababisha wakina mama kujifungulia nyumbani ni
kuwa na elimu ndogo na kutokujua umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya
na wengine wamekuwa na dhana ya kuwa hospitali hawezi kupata vitu ambavyo
wanavitumia kwenye mambo yao ya kishirikina hivyo hujikuta wanawalazimisha
wakina mama kujifungulia Nyumbani” Alisema Dr Kazuzu.
Bi Mery Musa ambaye ni mkazi wa Uyovu alisema tatizo kubwa ni
ukosefu wa elimu na vifaa kwenye baadhi ya zahanati hali inayosababisha wengi
wao kutoona umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya huduma za afya.
Akiwa kwenye ziara wilayani Bukombe, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi
Robert Gabriel alisema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma za afya
zinaboreshwa kwa kuwa na majengo ya kutosha na vifaa tiba pia.
No comments:
Post a Comment