Wednesday, 24 January 2018

RAIS MAGUFULI AOMBOLEZA KIFO CHA JAJI MSTAAFU WA MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufuatia kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Robert Kisanga kilichotokea jana tarehe 23 Januari, 2018 katika hospitali ya Regency Jijini Dar es Salaam.

Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Jaji Mstaafu Robert Kisanga atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa wakati wote wa utumishi wake uliojaa umakini, uchapakazi, uzalendo na ushirikiano na wengine, mambo ambayo yalimwezesha kupata mafanikio makubwa.

“Sote tunafahamu kazi nzuri alizofanya akiwa katika majukumu mbalimbali ya kitaifa, mchango wake katika kuijenga taaluma ya uanasheria baada ya uhuru na uanzishaji wa Mahakama ya Rufani baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, kwa hakika mchango wake hautasahaulika.

“Nakuomba Mhe. Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga, Majaji na wanasheria wote, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na amemuombea Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga apumzishwe mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Januari, 2018

No comments:

Post a Comment