Wednesday 22 June 2016

NI VITA YA KUNDI F URENO VS HUNGARY, RONALDO KUVUNJA MWIKO LEO?


Ureno leo wanakutana na Hungary kuwania nafasi ya kufuzu kuelekea hatua ya 16 bora katika mchezo wa kundi F utakaofanyika kunako dimba la Stade des Lumieres lililopo manispaa ya Lyon.

Kocha wa Hungary Bernd Storck anaweza kufanya ‘rotation’ katika kikosi chake kufuatia kujihakikishia nafasi ya kushiriki hatua ya 16 bora.
Hungary kwa mara nyingine tena watakuwa bila ya mchezaji wao Attila Fiola, ambaye ana majeraha ya kifundo cha mguu, hivyo beki wa kati Adam Lang atakuwa na jukumu la kuanza tena kama beki wa kulia.
Kocha wa Ureno Fernando Santos atasubiri ripoti ya daktari ili kujua kama ataweza kuwatumia beki wake wa kushoto Raphael Guerreiro na kiungo Andre Gomes – wote wakiuguza majeraha ya misuli.
Nahodha wa Ureno Cristiano Ronaldo anatarajia kucheza mechi ya 17 katika michuano ya Ulaya, akiweka rekodi mpya.
Hungary ni kama tayari wameshafuzu, ushindi ama sare ya aina yoyote katika mchezo wa leo utawahakikishia nafasi ya kwanza katika kundi F.
Ushindi kwa Ureno leo utawahakikishia nafasi ya kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano na watakuwa vinara wa kundi hilo vinginevyo Iceland nao washinde idadi kubwa ya mabao.
Kama Iceland na Portugal wote wakitoa sare, basi Iceland watamaliza nafasi ya pili labda ikitokea Ureno wawe na idadi nzuri ya mabao.
Mpaka sasa Ureno hawajawa na matokeo ya kuridhisha, sare mbili katika michezo yote ya awali. Wakipiga mashuti 49 na kufanikiwa kupata goli moja. Katika mashuti yote hayo, 19 yamepigwa nje ya lango, 15 yamelenga lango na mengine 15 yamezuiliwa. Hii inaweza kuwa hatari kwao endapo watafanya uzembe kwenye mchezo wa leo.
Akiwa amefunga magoli 364 katika michezo 348 na klabu yake ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ni mchezaji ambaye mara zote huwa na wastani mzuri wa kufunga – lakini ukame wake wa magoli katika michunao hii inaleta habari nyingine. Kati ya mashuti 20 aliyopiga katika michuano hii, manne tu yamelenga lango na hakuna lililofanikiwa kutinga wavuni.
Hungary hata wakipoteza mchezo wa leo bado wana nafasi ya kufuzu kwenda nafasi ya 16 bora kama ‘best loser’.
Kama wakishinda mchezo wa leo, basi wakutana na mshindi wa pili wa kundi E ambaye anaweza kuwa Ubelgiji, wakati ikiwa wakimaliza nafasi ya pili, maana yake watakutana na England. Na kama watamaliza ndani ya washindi watatu wa juu, basi watakutana na mshindi wa kundi C ambaye ni Ujerumani au kundi D. Hungary wameonesha kiwango kizuri mbele ya Austria na Iceland mpaka sasa, lakini kuanzia sasa kwenda mbele, mambo hayatakuwa rahisi kwa vijana hao wa Bernd Storck. Wanahitaji umakini mkubwa.
Takwimu za mechi walizokutana
Hungary hawajashinda mechi 10 mbele ya Ureno (sare 3, wamefungwa saba), wakishindwa kufunga goli katika michezo mitatu ya hivi karibuni waliyokutana.
Wamepoteza mechi zao zote tano za mwisho walizocheza na Ureno.
Mara ya mwisho kukutana katika michezo ndani ya michuano ilikuwa ni mwaka 1966, wakati Ureno waliposhinda 3-1 katika dimba la Old Trafford katika hatua ya mtoano.
Timu hizi zimepangwa kundi moja katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018, zitakutana Machi na Septemba mwaka 2017.
Hungary
Hungary wamepoteza michezo miwili kati ya 14 iliyopita (wameshinda mara 6, sare mara 6).
Mara ya mwisho kuvuka hatua ya makundi katika michuano mbalimbali ilikuwa ni kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1996.
Hawajawahi kushinda zaidi ya mchezo mmoja katika Michuano ya Ulaya.
Ureno
Ureno wamepiga jumla ya mashuti 49 katika michezo ya awali dhidi ya Austria na Iceland. Hakuna timu yoyote iliyopiga mashuti zaidi ya 36 katika mechi mbili za mwanzo.
Cristiano Ronaldo anatarajia kucheza mchezo wake wa 17 katika michuano hii, akivunja rekodi ya Lilian Thuram na Edwin van der Sar waliocheza michezo 16.
Ronaldo amepiga mashuti 20 katika michuano hii mpaka sasa, zaidi ya timu tisa katika michezo ya raundi ya pili. Hakuna mchezaji yoyote mwingine mwenye ‘attempts’ zaidi ya tisa katika michezo ya raundi mbili za awali katika michuano hii.
Akiwa na Ureno, Ronaldo amepiga faulo 36 katika michuano mbalimbali, lakini hajafunga hata moja mpaka sasa.
Ureno wamefanikiwa kuvuka hatua ya makundi katika mara zote sita zilizopita walizoshiriki michuano hii.
Wameshinda mara moja tu katika michezo yao sita iliyopita katika michuano mbalimbali (sare 4, wamepoteza mara moja).


No comments:

Post a Comment