Friday 17 June 2016

LEO NI VITA YA KUNDI E, ITALY VS SWEDEN EURO2016

Italy leo wanawania ushindi wa pili ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya Euro pale watakapokuwa na kibarua kigumu mbele ya Sweden, katika mchezo wa kundi E utakaofanyika kwenye uwanja wa Stade  de Toulouse uliopo manispaa ya manispaa ya Tolouse majira ya saa 10 jioni.

Italy maarufu kama Azzurri walionesha ukomavu wake katika mchezo wa awali uliochezwa Jumatatu dhidi ya Ubelgiji baada ya kushinda mabao 2-0, magoli yaliyofungwa na Emanuele Giaccherini na Graziano Pelle licha ya muda mwingi kuelemewa na wapinzani wao.
Ushindi wa leo utawafanya vijana hao wa Antonio Conte kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano na kuwasubiri wapinzani wao wengine watakaokuwa wakiwania nafasi ya kuungana nao.
“Nadhani nina kundi la wachezaji wenye akili nyingi mno katika kikosi changu, wengi wao wana hamu ya kuona tunafanya kitu chenye tija, na ndio maana tunapambana kuhakikisha tunavuka hatua hii ya makundi.” amesema Conte.
“Wanafahamu fika kwamba, tunapaswa kupambana kwa asilimia 100, kwasababu kama tuncheza kwa kiwango cha kawaida, tafsiri yake hatuwezi kupata matokeo. Ni lazima tufanye kitu cha ziad ili kuwafanya mashabiki wetu wajivunie timu yao.”
Kwa upande wa Sweden walianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Ireland, walipata goli dakika ya 71, goli ambalo Jamhuri ya Ireland walijifunga wenyewe.
Macho yote kwa siku ya leo tena yatakuwa kwa nahodha wa Sweden Zlatan Ibrahimovic ambaya anasaka kuwa mchezaji wa kwanza kufunga kwenye michuano minne mfululizo ya Ulaya na kumzidi Cristiano Ronaldo baada ya kushindwa kuonesha uwezo wake kwenye mchezo wa kwanza.
Lakini kocha wa Sweden Erik Hamren amemtetea nahodha wake huyo na kuwaasa wachezaji wake wote kwa umoja wao kucheza kwa badii kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi.
“Ili kuwa mshambuliaji bora, lazima upata sapoti kwa wachezaji wenzako. Safu yetu ya ushambuliaji haikuwa katika ubora unaohitajika. Ndani ya dakika 50 za mwanzo washambuliaji wetu hawakuwa wakipewa huduma nzuri.”amesema Hamren
“Tulianza kuingia mchezoni taratibu na kuanza kutengeneza nafasi. Ibrahimovic alihusika kwenye lile goli. Tunatakiwa kujitolea kwa asilimia 300 kwenye mechi zijazo kama tunataka kushinda.”
Takwimu muhimu kuelekea mchezo wa leo
Italy
Magoli saba kati ya tisa ya mwisho ya Italy dhidi ya Sweden yamefungwa katika kipindi cha kwanza.
Chini ya Antonio Conte, Italy hawajafungwa mechi 11 za ushindani (ushindi mara 8, droo tatu). Kipigo chao cha mwisho kilikuwa dhidi ya Uruguay wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 (wakati huo ikiwa chini ya Cesare Prandelli)

Katika michezo ya mwisho 34 ya michuano ya Ulaya, Italy hawajafunga zaidi ya magoli mawili.

Katika michezo yao 3 ya mwisho, Italy wamecha bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa.

Italy wamepoteza michezo miwili tu kati ya 22 katika hatua ya makundi ya fanali za michuano ya Ulaya (wameshinda mara 11, sare mara 9)

Antonio Candreva amehusika katika magoli matatu katika michezo miwili iliyopita kwa Italy (amefunga goli moja na kutoa assist mbili)

Sweden
Sweden wameshinda michezo yao mitatu tu kati ya 15 katika michuano ya Ulaya (sare 5 na kufungwa mara saba).

Licha ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Ireland, Sweden hawakupiga hata shuti moja lililolenga lango.

Zlatan Ibrahimovic anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mara nne katika michuano minne tofauti ya Ulaya kama atafunga leo. Mpaka sasa ana magoli sita katika michezo 11, ukijumlisha na ule dhidi ya Italy mwaka 2004.

Magoli saba ya mwisho ya Sweden yamefungwa na wachezaji saba tofauti (liliwemo moja la kujifunga).


No comments:

Post a Comment