Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Richard Kayombo akifafanua jambo alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari
kuhusu kodi za michezo ya kubahatisha leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Sehemu ya Huduma za Habari na
Picha Bw. Rodney Thadeus na kulia ni Mkuu wa Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TRA
Bi.Rachel Mkundai.
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakiendelea na kazi yao wakati wa mkutano baina yao na Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Richard Kayombo kuhusu kodi za michezo ya kubahatisha leo Jijini Dar es Salaam.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imeanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha kama
ambavyo ilikabidhiwa jukumu hilo kuanzia Julai Mosi 2017 kwa mujibu wa Sheria
ya Fedha ya mwaka 2017.
Hayo yameelezwa leo
jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw.
Richard Kayombo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa
kodi katika michezo hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Kayombo alisema kuwa
TRA inakusanya mapato katika michezo mbalimbali ya kubahatisha hapa nchini kama
vile Casino, Sport Betting, Slot Machines, Lottery na kupitia ujumbe mfupi wa
simu (SMS) na kusisitiza kuwa kiwango cha kodi kinatofautiana kati ya mchezo
mmoja na mwingine.
“Jukumu hili limetokana
na mabadiliko ya sheria ambayo yapo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 ambayo
imetupa mamlaka kamili ya kusimamia zoezi la ukusanyaji wa mapato katika
michezo ya kubahatisha,” alifafanua Kayombo.
Alibainisha kuwa kwa
wanaojihusisha na michezo hiyo katika Casino wanapaswa kuwasilisha TRA asilimia
15 ya mapato yatokanayo na mchezo huo kwa wiki na wanaochezesha michezo ya
Sport Betting wanatakiwa kuwasilisha asilimia 6.
Kayombo aliongeza kuwa
kwa wale wanaochezesha michezo hiyo kwa njia ya SMS wanatakiwa kuwasilisha
asimilia 30, kwa michezo ya kitaifa (National Lottery) wanatakiwa kuwasilisha
asilimia 10 na michezo ya slot machine wanatakiwa kuwasilisha sh. 32,000 kwa
mwezi kwa kila machine moja.
“Michezo ya kubahatisha
ina pande mbili yaani mchezeshaji na mchezaji hivyo kila mmoja anapaswa kulipa
kodi, ambapo mshindi wa mchezo huo pia anapaswa kulipa asilimia 18 ya mapato
yake ambayo hukatwa na mchezeshaji na kuiwasilisha TRA,” alisema Kayombo.
Aidha Kayombo alieleza
kuwa TRA itajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato tu, jukumu la kuratibu na
kuendesha michezo hiyo litabakia kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha hapa nchini
ambayo ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia michezo yote ya kubahatisha.
Alisema TRA
inashirikiana na Bodi ya Michezo hiyo katika kutoa elimu kwa wadau wote
wanaohusika na michezo ya kubahatisha wakiwemo wadhamini, wananchi, vyombo vya
habari na wadau wengine.
Pia TRA imetoa wito kwa
makampuni na wadau mbalimbali wanaohusika na michezo ya kubahatisha kuendelea
kutoa ushirikiano katika suala la ukusanyaji mapato yatokanayo na michezo hiyo
kwa ufanisi zaidi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 kama
ilivyopitishwa na Bunge.
Michezo ya Kubahatisha
inasimamiwa na kuendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Board of
Tanzania) ambayo mwanzoni ndiyo ilikuwa na jukumu la ukusanyaji kodi ambalo kwa
sasa limerudishwa TRA kwa mujibu wa Sheria ya Fedha Na. 4 ya mwaka 2017 baada
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuifanyia marekebisho.
No comments:
Post a Comment