Serikali
imelipongeza Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa
ushirikiano wake na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo hasa
katika sekta za Kilimo Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kutumia wataalam na
uzoefu kutoka Japan.
Pongezi hizo
zimetolewa Jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Msaidizi wa ushirikiano wa
kiufundi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Bw.Msafiri Marwa alipokuwa akiwaaga vijana wa kijapani waliokuwa
wanajitolea katika sekta ya Kilimo na Maendeleo ya jamii hapa nchini.
“Serikali ya Japan
kupitia shirika lake la JICA imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na serikali
ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile kuwajengea uwezo Watanzania
kupitia ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini Japan na kuleta watu wa
kujitolea katika miradi ya maendeleo hapa nchini,” alieleza Bw. Marwa.
Aidha, Bw.Marwa ambaye
alimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bi. Suzani Mlawi aliipongeza Japan
kwa kutumia rasilimali watu pamoja na rasilimali fedha kupitia JICA kufadhili
utoaji wa huduma za kijamii jambo ambalo ni kipimo cha ushirikiano kati ya nchi
hizi mbili.
Amewapongeza vijana wa
kijapan kwa kazi nzuri waliyoifanya hapa nchini katika kipindi chote cha miaka
miwili ya kuwahudumia watanzania hasa katika sekta ya Kilimo na Afya.
“Kwa niaba ya serikali
niwapongeze vijana wote mliokuja hapa nchini kwa kufanya kazi na jamii ya
Watanzania, mmefanya kazi kwa jitihada kubwa wakati mwingine katika
mazingira magumu, niwahakikishie kuwa serikali ya Tanzania itaendelea
kuimarisha mazingira ya ushirikiano ili kuendeleza uhusiano ” alifafanua Marwa.
Mkurugenzi huyo pia
aliwakumbusha vijana hao kuwa mabalozi wazuri nchini Japani na mataifa mengine
watakayokwenda ili kuwavutiwa wawekezaji na watalii kuja kuwekeza katika shughuli
za maendeleo pamoja na kuleta watalii wengi kwani Tanzania ina vivutio vingi
vya utalii, mazingira rafiki kwa wageni na amani ya kutosha.
Kwa upande wake,
Mratibu wa kundi la vijana wa kujitolea kutoka JICA Bw.Ichiro Owa alisema
kuwa, anaipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwapokea na kuwapa ushirikiano na
ulinzi wa kutosha vijana waliokuja kujitolea katika shughuli za maendeleo kwa
siku zote ambazo wamekuwa hapa nchini.
“Mpango wetu kwa sasa
ni kuleta vijana wengi zaidi wa kujitolea kwasababu ya ushirikiano tulioupata
kutoka kwa serikali ya Tanzania ni mzuri kwani tumefurahia usalama amani
na utulivu pamoja na ukarimu wa watanzania ” alifafanua Bw. Owa.
Mratibu huyo wa vijana
wa kujitolea kutoka Japan alisema ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania ni
wa kihistoria na umekuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, aliongeza kuwa
kwa mwaka huu, JICA ina jumla ya vijana 40 wanaojitolea na matarajio yao ni
kuongeza vijana kati ya 60 hadi 70 kwa mwaka ujao.
Vijana wa kujitolea
walioagwa katika hafla hiyo ni pamoja na Kyoko Tada aliyekuwa akifanya kazi ya
Uuguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Shu Sato aliyekuwa katika
Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro na Yusuke Sakakibara
aliyekuwa anafanya kazi ya maendeleo ya jamii katika Wilaya ya Masasi.
JICA ilianza mpango
wake wa kuleta vijana wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo
mwaka 1967 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tangu kuja kwa kundi la
kwanza kutoka Japani idadi imeongezeka kufikia vijana
1,568.
No comments:
Post a Comment