Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili akiwemo mlinzi wa Suma JKT
na mhudumu wa benki ya NBC tawi la Tangibovu ambao wanatuhumiwa katika tukio la
kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ),
Vincent Mritaba.
Kamanda wa kanda hiyo,
Lazaro Mambosasa amesema leo Jumatano kuwa Septemba 11 mwaka huu saa 11 jioni
maeneo ya Tegeta Masaiti jeshi hilo lilipata taarifa ya Mritaba kuvamiwa na
watu wawili wasiojulikana ambao walimjeruhi na kumpiga risasi ya begani, tumnoni
na kwenye paja la mkono wa kulia huku wakimpora kiasi cha Sh5 milioni.
Amesema tukio hilo
lilitokea baada ya mstaafu huyo kutoka kuchukua fedha hizo katika benki ya NBC
tawi la Tangibovu akiwa kwenye gari lake ya Volkswagen Amarok.
Mambosasa amesema alipofika
nyumbani kwake alipiga honi na kufunguliwa geti na mlinzi wake Godfrey Gasper.
Amesema geti
lilipofunguliwa pikipiki ilisimama hapo getini na watu wawili waliokuwa wamevaa
helment walishuka na kulifuata gari huku wakiwa na silaha aina ya bastola ndipo
walishambulia upande wa kulia wa dereva na katika kioo cha mbele.
"Huku
wakimwamuru ashuke ambapo risasi zilimjeruhi maeneo ya begani, tumboni na
kwenye paja la mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia pikipiki
waliokuja nayo," alisema Mambosasa.
Mambosasa amesema cha
kushangaza wakati mlinzi huyo anaenda kufungua geti silaha yake aina ya shotgun
yenye namba TZCAR9644 aliiacha kwenye kibanda cha ulinzi huku ikiwa chini ya
kitanda.
Amesema baadaye
watuhumiwa walimwambia akimbie katika eneo hilo na yeye alitii amri hiyo na
kwenda mbali na tukio hilo jambo ambalo linatia shaka.
"Ninavyojua
askari wa Suma JKT anapewa mafunzo ya ukakamavu haiwezekani uache silaha chini
ya kitanda unakwenda kufungua geti kitu ambacho sikubaliani nacho,"alisisitiza
Amesema walipofuatilia
mawasiliano ya mmoja wa wahudumu wa benki hiyo walibaini kuwa alikuwa anapanga
mipango na watu mbalimbali wanaokwenda katika benki hiyo. Hivyo msako mkali
unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika katika tukio la kujeruhi kwa
risasi afande huyo.
Pia alizungumzia
kuvunjwa kwa ofisi ya wakili ya Prime Attoneys akieleza kuwa wanaendelea na
msako mkali ili kuwabaini waliohusika katika tukio hilo na watakapokamatwa
watachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment