Jaji Mkuu wa Kenya,David Maraga ametua nchini katika mkutano wa
majaji na mahakimu akionekana kivutio kwa wengine.
Jaji huyo ni mmoja wa majaji wakuu 13 kutoka nchi mbalimbali
duniani wanaohudhuria mkutano majaji na mahakimu wa nchi za Jumuiya ya Madola
unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu..
Maraga amegeuka kivutio baada ya kushangiliwa na majaji
waliohudhuria mkutano huo wakati alipotambulishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Profesa Ibrahim Juma.
Profesa Juma amempongeza Maraga kwa kuwakilisha mfano bora wa
kulinda uhuru wa Mahakama kwa nchi nyingine duniani.
Kiongozi huyo ameonekana akiwa ameambatana na walinzi wanne
ambao wanamfuata popote anapotembea nje ya mkutano huo.
Hata hivyo, Maraga amekataa kuzungumza na vyombo vya habari kwa
madai amekuja kuhudhuria mkutano huo na siyo kwa jambo jingine lolote.
Mkutano huo umefunguliwa leo Jumatatu na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu ukiwa na kauli mbiu "Kujenga Mahakama Shirikishi, Thabiti na
Inayowajibika."
Jaji Maraga kwa siku za hivi karibuni amekuwa maarufu baada ya
kutoa uamuzi wa kufuta Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliokuwa umempa ushindi Rais
Uhuru Kenyatta.
No comments:
Post a Comment