Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha
Serikali
imepanga kuongeza idadi ya Maafisa Ugani wenye ujuzi katika kila Kata na
Kijiji ili kuleta mapinduzi ya kilimo Nchini.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha wakati akijibu
swali lililohusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inafanya mapinduzi ya
kilimo kwa kuwa na wataalamu wa kutosha, leo Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri huyo
amesema kuwa Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye
kuajiri watanzania wengi hivyo mapinduzi ya kilimo yatachangiwa na uwepo wa
wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze kushauri matumizi
ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
" Hadi kufikia
mwaka 2016/2017 Serikali imeajiri maafisa ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya
mahitaji ya maafisa ugani 20,374 katika ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya"
amefafanua Naibu Waziri Ole Nasha.
Aidha, Naibu Waziri
Ole Nasha aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha na kuwezesha vituo vya
kilimo na vituo vya Rasilimali za kilimo za kata (WARCs) kwa ajili ya
kufundishia teknolojia mbalimbali za kilimo.
Vilevile alisema kuwa
Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo na mafunzo ya
huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za Ugani na
kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima nchini.
Mbali na hayo Serikali
inaendelea kusomesha vijana na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali
fedha.
No comments:
Post a Comment