Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga akiongea na
waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya kukamatwa kwa kamati ya Ujenzi wa
vyoo vya shule ya msingi Bariadi baada ya kutafuna mil 4.8
Vyoo vya awali vya shule ya msingi Bariadi.
Mkuu wa shule ya Msingi Bariadi Mayila Ndalahwa
akihojiwa na waandishi wa habari juu ya sakata la vyoo na uhitaji
kwa wananfunzi wa shule hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Festo Kiswaga ameliagiza Jeshi
la Polisi wilayani humo kuwakamata na kuwaweka rumande watu watano ambao ni
Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Msingi Bariadi, baada ya kudaiwa kutumia vibaya
fedha za ujenzi wa matundu 14 ya vyoo vya shule hiyo zilizotokana na michango
ya wananchi.
Kamati hiyo inadaiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 4.8 ambazo
zilichangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi huo ili kupunguza uhaba wa matundu
ya vyoo uliokuwa unaikabili shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1373.
Kiswaga aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mlela Hosea mwenyekiti wa kamati
ya ujenzi, Lucas Gervas Makamu Mwenyekiti, Kenedy
Machume, Wodya Husein na Suzan Ezekiel ambao ni wajumbe wa
kamati hiyo.
Kiswaga aliwaonya wote wenye tabia ya kugusa fedha zinatokana na michango
ya wananchi kuwa serikali yake itawashughulikia ipasavyo kwa kuwakamata na
kuwafikisha mahakamani, na kuwataka wananchi waendelee kuchangia fedha kwa
ajili ya kujiletea maendeleo.
Akizungumzia suala hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bariadi
Mayila Ndalahwa anasema dalili za wajumbe hao kufuja fedha zilizochangwa na
wananchi kwa ajili ya ujenzi wa vyoo zilianza kuonekana mapema baada ya
kumfukuza fundi aliyekuwa ameidhinishwa na mkutano mkuu wa wazazi.
‘’Kila mzazi alichangia Elfu 7600
ili kufanikisha ujenzi huo, na kamati hiyo ilitokana na wazazi
wenyewe…ilionekana walianza kununua vifaa hewa kwa sababu walikuwa wakichukua
fedha nyingi lakini wanaleta vifaa vichache, mfano saruji’’ alisema
Ndalahwa.
Wanafunzi wa darasa la sita Anastazia Pius na Emanuel Amos walisema
wamekuwa wakikutana na foleni kubwa chooni kutokana na msongamano mkubwa wa wanafunzi
sabau ya upungufu wa vyoo kwa sababu wanafunzi ni wengi tofauti na mahitaji ya
vyoo.
Mmoja wa wazazi aliyekuwa Shuleni hapo Mathias Sakagoi alisema kuwa
walichangia ujenzi huo tangu mwezi February lakini hadi sasa umesimama bila
taarifa na hali iliyoawasababisha kutohudhuria vikao vya shule baada ya kubaini
ubadhirifu uliokuwa ukifanyika.
Shule ya msingi Bariadi ina jumla ya wanafunzi 1373, ina matundu 12, na
upungufu wa matundu 57 kwa sasa inakabiliwa na tatizo la uhaba wa matundu ya
vyoo kwa muda mrefu ambapo wazazi waliamua kuchangia ujenzi huo ili kuwanusuru
wanafunzi hao.
No comments:
Post a Comment