Rais John Magufuli
ameagiza kujengwa uzio katika eneo linalozunguka machimbo ya Tanzanite liliko
Simanjiro ikiwa ni hatua yake ya kutaka kukabiliana na utoroshwaji wa
rasilimali hiyo.
Amelisisitiza Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
Rais Magufuli ambaye
yuko ziarani mkoani Manyara amesema vikosi vya ulinzi na usalama vinapaswa
kushirikiana kujenga ukuta huo ambao utaanzia eneo la block A hadi D la
machimbo hayo.
Baada ya ujenzi huo
kukamilika ametaka kufungwa mitambo maalumu ikiwamo kamera zitakazokuwa na
uwezo kutambua na kubaini matukio yoyote yanayotendeka katika eneo hilo.
“Nataka ukuta huu uanze mara moja
tena JWTZ kupitia Suma JKT waanze kazi hii mara moja na baada ya kukamilika
eneo hili liwe na mlango mmoja tu ambao utaweka mtambo wa ukaguzi... wewe
ukiweka Tanzanite tumboni tutakubaini, ukiweka kwenye kiatu uonekane pia,”
alisisitiza Rais Magufuli.
Amesema lengo la
Serikali kufanya hivyo ni kuhakikisha inapata sehemu ya mapato yake na
wawekezaji waondoke na haki yao bila kupunjwa upande wowote.
Amesema hataki kuona
rasilimali za Taifa zinatoroshwa kienyeji na kwenda kuwafaidisha wajanja
wachache walioko nje ya nchi hivyo ili kudhibiti hali hiyo ameamua kuchukua
hatua madhubuti.
“Hapa adui yetu siyo CCM au
Chadema ama mwingine yeyote, adui yetu ni yule anayopora mali zetu, hatupaswi
kugombana sisi wenyewe na kumuacha adui yetu yuko pembeni, naomba tushikamane
katika hili maana hii vita ya uchumi siyo lelemama lazima tuwe wamoja,”
alisema.
Pia, amesema ndoto
yake ni kuona soko la Tanzanite linakuwa Simanjiro ili wafanyabiashara kutoka
ng’ambo kama Marekani, India na Ulaya wanafika kwenye eneo hilo kufanya
biashara.
“Tunataka soko la
Tanzanite linakuwa hapa Simanjiro ili hawa wafanyabiashara wafunge safari waje
kununulia hapa na hiyo itakuwa na manufaa pia kwa wafanyabiashara wa eneo hilo
maana hata yule mchinja mbuzi ama mwenye gesti atafaidika na ujio huo,” aliongeza
Rais Magufuli amesema
hayo leo Jumatano wakati akizindua barabara ya kiwango cha lami ya Mererani
yenye urefu wa kilometa 26 ambayo imegharimu kiasi cha Sh 32.5 bilioni.
Rais ameahidi kuendelea na kipande kilichobakia ili lami hiyo ifike makao makuu
ya Mkoa wa Manyara ambayo ni Babati.
No comments:
Post a Comment