Kigango cha Kanisa Katoliki la mtakatifu Petro
katika kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu.
Paroko wa Parokia ya Ngulyati Padri John Nkinga
akiwa kwenye maadhimisho ya misa takatifu ya kipaimara kijiji cha Gamboshi.
Mhashamu askofu Liberatus Sangu wa Jimbo la Shinyanga akiongoza
maadhimisho ya misa takatifu ya kipaimara ambapo waimarishwa 200 walipewa
kipaimara Gamboshi, huku akiwataka viongozi wa serikali kulitazama eneo hilo
hasa kupeleka elimu ili kuibadili jamii hiyo iliyokuwa inasifika kwa ushirikina.
Diwani wa kata ya Gamboshi Bahame Kaliwa akiongesa
na waumini na wananchi waliohudhuria katika adhimisho la misa hiyo juzi, na
kusema kuwa eneo hilo ni salama, lakini linakabiliwa na uhaba wa miundombinu ya
elimu.
Askofu Liberatus Sangu akiwapa kipaimara waumini wa kanisa hilo la Gamboshi ili kuwaimarisha kiroho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi mkoani Simiyu
Wananchi wa Kata ya Gamboshi wilayani Bariadi mkoani Simiyu wamemwomba
waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kufika katika
kijiji hicho ili kutatua changamoto za kielimu zinazolikabili kijiji hicho. na
kulifanya kuwa nyuma kimaendeleo.
Mbali na Waziri huyo, Viongozi wengine ambao wamekuwa wakiogopa kufika
eneo hilo kutokana na historia yake kuwa ni kijiji cha wachawi wameombwa kufika
na kutatua changamoto hizo ili kuifuta dhana iliyokuwa imejengeka kuwa ni
ki jiji cha wachawi.
Akiwasilisha maoni hayo ya wananchi kwenye misa ya kipaimara
iliyoadhimishwa kijijini hapo, Diwani wa kata hiyo Bahame Kaliwa amemtaka
waziri huyo kufika ili kujionea changamoto za kielimu hasa wingi wa wanafunzi
madarasani na pia ajionee miundombinu duni ambayo hawawezi kuimaliza
kwa haraka.
‘Hii dhana ya ushirikina
iliyokuwa imejengeka haiwezi kuondolewa bila elimu…hivyo tunamwomba waziri wa
elimu tunamwomba afike hapa aje aone watoto walivyowengi, na aone miundombinu
ilivyoduni ambayo haiwezi kuondolewa kwa uharaka, hasa neno lililojengeka la
ushirikina’ alisema Kaliwa.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu
amewataka viongozi wa serikali kuyafikia maeneo ambayo yalikuwa yamesahaulika
ikiwemo Gamgoshi, na kuyapelekea miundombinu na kuwafungua watu hao ili waweze
kubadilika kifikra, kimaono na kimtazamo.
Sangu aliongeza kuwa ikiwezekana wanafunzi wote waliohitimu elimu ya
msingi kijijini hapo wawe wamefaulu au hawajafaulu waende sekondari ili baada
ya kuhitimu waweze kuibadilisha jamii ya eneo hilo, na kuwafungua wapate elimu.
’Viongozi wa ngazi za Serikali waje kuyafikia
maeneo haya, wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba waende wote sekondari
hata kama hawajafaulu ili kuibadili jamii yao iweze kuondokana na ukatili wa
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa sababu wote wamezaliwa na kuumbwa kwa
sura na mfano wa mungu’ alisema Sangu.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria Maadhimisho ya misa hiyo takatifu ya
kipaimara walisema kuwa eneo hilo kwa sasa ni tulivu tofauti na inavyoaminika
kwa sababu ni sawa na maeneno mengine ya nchi na watu wanaoishi huku ni wa
kawaida sana, alisema Danieli Mvungi kutoka Morogoro aliyekuwa amehudhuria misa
hiyo.
Padri wa parokia ya Ngulyati John Nkinga alisema kuwa hadi sasa kuna
mabadiliko makubwa kutokana na watu wa eneo hilo wameanza kubadilika kiimani
kwa kumcha mungu, ambapo jumla ya waimarishwa 200 walipewa kipaimara katika
kanisa la Mtakatifu Petro Gamboshi.
No comments:
Post a Comment