Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Bw. James Kilaba (katikati)
akiandika maoni ya wadau wa mitandao ya blogu na Online Tv wakati wa uzinduzi
wa kampeni ya kusisitiza matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa awamu ya pili
mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mamlaka ya Mawasiliano
nchini(TCRA) imetia nia kuboresha mawasiliano kwa umma hasa katika matumizi ya
mitandao ya kijamii ili kuwawezesha watanzania kupata elimu bora ya maendeleo
na kujenga uchumi uliobora.
Haya yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na
Mwenyekiti wa Bodi wa Mamlaka hiyo Dkt. Jonas Kilimbe alipokua akihutubia hadhara ya wamiliki wa
vyombo vya habari mtandaoni (blogu na Online TV) katika uzinduzi wa kampeni ya
awamu ya pili ya “kusisitiza matumizi bora ya mitandao ya kijamii” iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere.
Katika hafla hiyo, Dkt. Kilimbe alisema kuwa kwa sasa
teknolojia ya mtandao inakua kwa kasi kwa hiyo huduma za habari zinapatikana kila
sehemu kwa njia ya mtandao na kufanya matumizi ya mitandao kuwa makubwa.
“Sekta ya mawasiliano kwa umma imepiga hatua kubwa
sana duniani kwa sasa, kwa kiasi kikubwa mtandao unachangia kuwepo kwa habari
nyingi. Tanzania inajumla ya televisheni za mitadaoni zipatazo 50 pamoja na
blogu 150 ambazo zote zinatoa taarifa kwa wananchi, hii inaashiria kuwa
mawasiliano kwa umma yamehamia zaidi kwenye mtandao”, alisema Dkt.Kilimbe.
Aidha Dkt.Kilimbe alisema kuwa sekta hii inapaswa
kuangaliwa zaidi kwani ni sekta muhimu kwa ujenzi wa Taifa na kuwaasa vijana
kutumia vizuri teknolojia hiyo kwa kujielimisha kuhusiana na masuala ya
maendeleo kuliko kutumia vibaya mitandao hiyo.
“Tuna jukumu zito na ni kubwa kwa sababu sekta hii
ya mawasiliano imeshikiria kila kitu na tasnia ya habari ina nguvu kubwa sana
kwa kuleta elimu ya maendeleo kwa wananchi kwa hiyo waandishi mitandaoni
tumieni weledi mkubwa kwa habari za
maendeleo.”, alisisitiza Dkt. Kilimbe.
Dkt.Kilimbe alisema kuwa katika matumizi ya
teknolojia hii mpya yanapaswa kuzingatiwa
kwa ajili ya ujenzi wa taifa hasa kwa wale wanaotumia vizuri mitandao ya
kijamii inawapa elimu kubwa ya maendeleo.
Aidha Dkt. Kilimbe amekishukuru chama cha wamiliki
wa blogu na televisheni mtandaoni(TBN) kwa kuleta umoja na kuzingatia maadili
na weledi wa umilikajia wa vyombo hivyo kwa kuwahabarisha wananchi.
Naye mtoa mada na mwakilishi kutoka TCRA Bw. Thadeus
Lingo alisisitiza usalama wa matumizi ya mtandao akisema kuwa idadi ya
watumiaji wa mitandao imeongezeka duniani kuanzia Julai 1, 2017 na kufikia
bilioni 3.8 huku kati ya hao bilioni 3.4 ambayo ni sawa na asilimia 92 ni
watumiajia wa mitandao ya kijamii hali iliyosababisha kuongezeka kwa vyombo vya
habari kuhamia mtandaoni, kwa hiyo weledi unahitajika katika kuhabarisha umma
kwa njia hii.
Kwa upande wake mratibu masaidizi wa polisi kitengo
cha makosa ya kimtandao (Cybercrime) Bw.Joshua mwangasa alisema kuwa watumiaji
wa mitandao ya kijami wanapaswa kutumia mitandao hiyo kwa makini zaidi ili
kujiletea maendeleo na kuepusha matumizi ya lugha za matusi.
Akizungumzia sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka
2015 katika kifungu kidogo cha 16 kinachoelekeza kuchapisha habari za uongo
mtandaoni kuwa ni uvunjaji wa sheria hiyo.
Mwangasa alisema kuwa kuanzia mwaka 2015 zaidi ya
kesi 5172 ziliripotiwa huku mwaka 2016 kesi 7889 zilipelekwa mahakamani kwa
kusikilizwa zaidi lakini mwaka 2017 kesi zilikuwa 3346 zimefikishwa mahakani na
kituo cha polisi.
Aidha mwangasa ameeleza kuwa anga la mawasiliano kwa
Tanzania liko salama kwa matumizi ya wanahabari na watanzania kwa ujumla.
“Anga letu la cyberspace ni salama sana
ukilinganisha na nchi zingine za ukanda wa maziwa makuu kwa hiyo tutumie fursa
hii kwa kujiletea maendele na siyo kutumia kwa uharifu wa matusi na lugha
zingine za kejeli”, alisema Bw,Mwangasa.
No comments:
Post a Comment