Waziri mkuu Kassim
Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba nchini wahakikishe
wanasimamia vizuri wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kuwaletea
tija wananchi.
Agizo hilo limetolewa
Jumanne, Septemba 26, 2017 na Waziri Mkuu wakati akizungumza na wakuu hao wa
mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dar es Salaam kujadili maendeleo ya zao
hilo.
Kikao hicho ni
muendelezo wa kikao alichokitiisha mjini Dodoma (Ijumaa, Septemba 8, 2017)
kujadili mbinu za kufufua zao hilo.
Wakuu wa mikoa
walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera,
Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi, Kigoma na Geita.
Waziri Mkuu amesema
katika kipindi hiki ambacho msimu wa maandalizi ya kilimo cha pamba umeanza ni
vema kwa Maofisa Kilimo na Wagani wakawasimamia wakulima kwa ukaribu ili
wahakikishe wanafuata mbinu bora za kilimo.
Amesema iwapo wakulima
watapata usimamizi mzuri kutoka kwa Maofisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao
kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba yao itawasaidia katika
kuongeza tija, kwenye uzalishaji wao.
“Serikali inawataka
Maofisa Kilimo na Wagani wawasimamie wakulima kuanzia maandalizi ya shamba,
kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko ili kilimo cha
zao hilo kiweze kuwaongezea tija.”
Amesema Maafisa Kilimo
wote walioko kwenye kila Halmashauri ni lazima wahusike kikamilifu katika
kuwaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu bora za kilimo ili waweze kupata
mazao mengi , hivyo kujikwamua kiuchumi.
Pia Waziri Mkuu
amewaagiza Wakuu wa Vyuo vya Kilimo nchini wahakikisha wanakuwa na mashamba
darasa yatakayotumika na wakulima na wanafunzi wao kujifunza mbinu bora za
kilimo kwa vitendo.
Kikao hicho kilihudhuriwa
na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya
Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito
Haule na Mkurugenzi Uhamasishaji Mazao, Bw. Twahir Nzallawahe.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
No comments:
Post a Comment