Monday 6 February 2017

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NI YETU SOTE- RAIS MAGUFULI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya ulinzi kuendeleza vita dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya  kuwaapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali James Aloyce Mwakibolwa.

Rais amesema kuwa kitendo cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Ernest Mangu kuwasimamisha baadhi ya watendaji kazi wake kimeipa heshima jeshi la polisi nchini.

“Madawa ya Kulevya yanapoteza nguvu kazi za watanzania hasa vijana, hivyo hii kazi si ya mtu mmoja ni ya wanzania wote kushirikiana kwa pamoja katika kupambana na jambo hili kwa manufaa ya nchi” alifafanua Rais Magufuli.

Mbali na hayo alisema kuwa, katika mapambano vipo vikwazo kadha vitakavyojitokeza hivyo watanzania wanabudi kuungana kwa pamoja dhidi ya wafanyabiashara wa madawa ya kulevya.

Katika hatua hiyo Rais Magufuli alisema kuwa kwa sasa nchi inavyoelekea katika uchumi wa kati kupitia viwanda, amelitaka Jeshi la Ulinzi nchini kusimamia na kujenga nchi ya viwanda kwa vitendo.

“haiwezekana Tanzania ya leo bado inaagiza sare kutoka china,wakati nchi yetu ina wakulima wazuri wa pamba, hivyo vyombo vya ulinzi mnatakiwa kujipanga katika hili, mkiamuua kuzungumza na baadhi ya viwanda na kuwapa vipimo na ubora wa nguo, rangi watatengeneza. ”alisema Rais Magufuli.
Alisema kuwa si kila kitu lazima kununua kutoka nje, ni lazima kujipanga kwa kuhakikisha dhana ya viwanda inaanzia jeshini.

“Tubadilike tutengeneze Tanzania kwanza, maslahi ya nchi yapewe kipaumbele, rasilimali zilizopo zitumike kwa manufaa ya nchi” alisisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua hiyo Rais Magufuli alitoa wito kwa majeshi nchini kutoa ushirikiano kwa wateule, kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa manufaa ya nchi na askari wengine.

Kwa upande wake Rais wa Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Ali Shein alisema kuwa jeshi la Tanzania linasifa kubwa ndani na nje ya nchi hivyo anaamini wateule wapya watafanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa.

Naye Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, ajali ya milipuko ya mabomu yaliyotokea Mbagala na Gongola mboto ndio kilikuwa kipindi kigumu kwake kwani watu waliumia na mali za wananchi na za jeshi zilipotea.

Wakati huo Jenerali Mkuu wa Majeshi aliyeapishwa leo Venance Mabeyo ameahidi kuendeleza na kuimarisha ulinzi wa taifa la Tanzania pale ambapo Jenerali Mstaafu Mwamunyange alipoishia na kama ilivyo majukumu ya jeshi kimsingi.

Rais Magufuli pia aliwaapisha Kamishina Jenerali wa Magereza Dkt Juma Alli Malewa ambaye alikuwa Kamishina wa Sheria na Uendeshaji wa Taifa la Magereza.

Wengine ni Balozi Paul Mella ambaye ataiwakilisha nchi ya Tanzania nchini katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Balozi Samweli William Shelukindo ambaye anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ufaransa pamoja na Nyakimura Mathias Mhoji ambaye amekuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.


Naye Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu amemuapisha Kamishina wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

No comments:

Post a Comment