Wednesday 15 February 2017

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YAPOKEA MSAADA WA PIKIPIKI 14



Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepokea msaada wa pikipiki 14 zenye thamani ya shilingi milioni 66 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ukusanyaji takwimu sahihi kwenye baadhi ya mikoa
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi.Nadia Belhaji Hassine alisema lengo la kukabidhi msaada huo ni kuboresha kazi ya ukusanyaji takwimu mikoani hasa sehemu ambazo hazifikiwi kwa usafiri wa gari.

Bi. Hassine amesema kutokana na kazi inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kufanikisha ukusanyaji na usambazaji wa takwimu mbalimbali ambazo zimekuwa na matokeo chanya taasisi hiyo imeamua kutoa msaada huo ili kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo uweze kuwa bora zaidi.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano hayo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema msaada huo utaboresha na kukuza tasnia ya takwimu ili kuweza kupata taarifa muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Dkt Chuwa alisema msaada huo utarahisiha usafiri wa kutoka eneo moja la utafiti hadi lingine na kuweza kusaidia katika upatikanaji wa taarifa muhimu za kitafiti.

Akipokea moja ya pikipiki hizo Bw.Lugome Kalisto kutoka Ofisi ya Takwimu Mkoa wa Pwani aliishukuru Benki ya Dunia kwa msaada wa pikipiki hizo kwani wamekuwa wakipata shida ya usafiri katika ukusanyaji wa takwimu hasa maeneo ambayo usafiri wa gari haufiki.


”Tumekuwa tukipata shida katika ukusanyaji wa takwimu hasa maeneo ambayo hayafikiki kirahisi kwa gari hali ambayo imekuwa ikifanya utendaji wetu kuwa duni.Alisema Bw. Kalisto.

No comments:

Post a Comment