Tuesday 7 February 2017

ADA ZA UHAKIKI WA FILAMU ZIPO KWA MUJIBU WA SHERIA



Ada za uhakiki wa filamu hapa nchini zipo kwa mujibu wa sheria na kanuni, ambapo gharama hizo hulipwa kwa nakala mama na baada ya hapo mtayarishaji huzalisha nakala kwa idadi anayohitaji.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Anastazia Wambura ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi juu ya Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama za ukaguzi ambapo kwa hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja kwa dakika.

“Nchi yetu hutoza ada ambazo ni rafiki ukilinganisha na nchi nyingine, kwa mfano, Nigeria ambayo ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwa upande wa filamu, hutoza filamu yenye urefu wa dakika 60 (filamu ya lugha asili) Naira 30,000 sawa na zaidi ya dola 150 ambayo ni sawa na Sh. 337,950 za Kitanzania na Kenya, ni sawa na Sh. 190,000,” alifafanua Anastazia Wambura.

Aliendelea kwa kusema kuwa Tanzania hutoza filamu za Kitanzania zenye urefu wa dakika 60 kwa Sh. 60,000 (sawa na Sh. 1,000 kwa dakika) ambapo gharama hizo ni sawa na asilimia 18 ya gharama za Nigeria na asilimia 32 ya Kenya.
Hivyo basi Tanzania imekuwa ikitoza ada hiyo ya uhakiki wa filamu kwa gharama nafuu na rafiki ukilinganisha na nchi nyingine Afrika.

Akijibu swali la namna gani Bodi hiyo imejipanga kuhakikisha huduma zao zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo wasanii wachache ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu ya Bodi hiyo, Wambura amesema kwamba Bodi hiyo imeendelea kujitangaza kwa wadau kupitia shughuli mbalimbali za kitaifa na Kimataifa kama vile kushiriki katika maonesho ya Sabasaba.

Vile vile bodi hiyo imekuwa ikishiriki katika wiki ya Vijana na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festivals (JAMAFEST). Pia hutumia vyombo mbalimbali vya habari kama vile TBC1, E-FM, Clouds media pamoja na magazeti mbalimbali kueleza watanzania kazi zinazofanywa na Bodi hiyo.


Aidha Bodi hiyo imekuwa ikifanya warsha za kuwajengea wadau wake weledi katika masuala ya filamu sehemu mbalimbali ikiwemo mikoani na  wilayani ikiwa ni moja ya maeneo ya kujitangaza.

No comments:

Post a Comment