Monday 6 February 2017

RAIS MAGUFULI ATAKA VITA YA UNGA ISIJALI UMAARUFU



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kuwataka viongozi wa majeshi nchini kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa madawa ya kulevya bila ya kujali nafasi zao, na umaarufu wao.
Akizungumza baada ya kuwaapisha Mkuu wa Majeshi nchini na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Rais Magufuli amesema hakuna cha mtu maarufu wala mtoto wa kiongozi, yeyote akikamatwa afikishwe mahakamani na kuagiza mahakama kuharakisha kutoa hukumu zinazohusu dawa za kulevya.

Pia amesema hata kama ni mke wake, naye anatajwa kuhusika na dawa za kulevya, akamatwe haraka na apelekwe mahakamani. 

"Hakuna cha mtu Maarufu Mwanasiasa, Waziri, au Mtoto Wa Fulani hata mke wangu akijihusisha hapa peleka maana madawa ya kulevya yamefikia pabaya" Amesema
Amesema vita hii asachiwe mtu mmoja bali ni ya jamii nzima huku akifafanua umuhimu wa kuanza kukamata watumiaji

"Hii vita si ya Makonda peke yake bali ni ya watanzania wote, shika yeyote peleka mahakamani na ndiyo maana nazungumza hakuna cha umaarufu, mkishika hawa wote wanaovuta madawa ya kulevya wataeleza nani aliwauzia, na huyo aliyewauzia ataeleza ameyapata wapi na huyo naye ukimshika ataeleza ameyapata wapi, lazima mtengeneze hiyo chain yote ili kuhakikisha wote wanaohusika na madawa ya kulevya wanashugulikiwa kikamilifu" alisema Rais Magufuli 

Pia Rais Magufuli amekiri kuwa anafahamu kuna watu walikuwa wanampigia simu IGP Ernest Mangu na kumpa ushauri juu ya mambo ya madawa ya kulevya, hivyo Rais amesema kama angejaribu kuwasikiliza basi leo asingekuwa na hiyo nafasi tena.

"Najua mtapata vipingamizi fulani, nafahamu kuna watu walikupigia simu IGP kukushauri shauri juu ya madawa ya kulevya, nashukuru hukuwasikiliza, ungewasikiliza ningejua na wewe unahusika, na leo usingekuwa IGP" alisema Rais Magufuli. 

Kauli hii ya Rais Magufuli inakuja ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda atangaze vita dhidi ya watu wanaohusika na dawa za kulevya akianza kwa kutaja majina yakiwemo ya askari na ya wasanii maarufu wa muziki na filamu akiwemo Wema Sepetu, Chid Benz, Vanessa Mde n.k.


Siku tatu baada ya Makonda kuwataja watuhumiwa hao, IGP Ernest Mangu alichukua hatua ya kuwasimamisha askari  12 waliotajwa na kuahidi kuchukua hatua zaidi, jambo ambalo limepongezwa na Rais Magufuli na kumueleza kuwa endapo asingechukua hatua hiyo, angejua kuwa na yeye anahusika.

No comments:

Post a Comment