Wednesday 8 February 2017

SITAKUBALI TANESCO KUPANDISHA BEI YA UMEME - PROF. MUHONGO



Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa msimamo wake juu ya  Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutopandisha gharama za umeme kwa wateja wake upo palepale.
Prof. Muhongo ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja zilizowasilishwa na wabunge  juu ya zuio la upandishaji bei ya umeme kwa shirika hilo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya shughuli za Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika kipindi cha mwaka  2016/2017.

“Haiwezekani wakapandisha bei ya umeme wakati kuna watu ndani ya Shirika wanamiliki hadi hoteli nne, wakijaza lita 20 za mafuta  katika magari wanaandika lita 50 na kila mwisho wa mwaka wanagawana milioni 50 kama ‘bonus’,” alifafanua Prof. Muhongo.

Ameendelea kwa kusema kuwa Shirika hilo linadaiwa kiasi cha shilingi Bil. 820, katika deni hilo kiasi cha shilingi Bil.320 bado hazijachambuliwa. Hivyo shirika hilo haliwezi kujiamulia kupandisha gharama ya umeme wakati huo huo wakiwa bado hawajachambua baadhi ya madeni yao.

Aidha Prof. Muhongo amesema kuwa, Shirika hilo linahitaji kiasi cha Dola Bil. 12 kwa ajili ya uwekezaji ili ifikapo mwaka 2020 kiasi cha Mg 5000 za umeme ziweze kuzalishwa.

Hata hivyo, Prof. Muhongo amesema amekwisha anza kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia ili kuona kama wataweza kufadhili kiasi hicho cha fedha ili kiweze kuwekezwa katika Shirika hilo.


Aliendelea kwa kusema kuwa Shirika hilo linahitaji mabadiliko ya hali ya juu ili kulifanya kuwa la kisasa na kuendana na dhima ya nchi ya  uchumi wa viwanda ambao kwa asilimia kubwa unahitaji nishati hiyo ya umeme.

No comments:

Post a Comment