Monday 6 February 2017

MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA YATOA MIKOPO KWA ZAIDI YA VIKUNDI 309



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde

Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi 1,867,896,520 kwa vikundi vya vijana 309 katika Halmashauri 94.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge  wa Viti Maalum Zainab Katimba alipotaka kujua idadi ya vijana walionufaika kupitia mfuko huo na namna ambavyo mikopo hiyo imebadilisha maisha yao.

“Lengo la kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini (Tanzania Bara) kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali,” alifafanua Mavunde.

Aliendelea kwa kusema kuwa fedha za mikopo zitokanazo na Mfuko huo umekuwa msingi mzuri katika kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine na hata kukuza vipato vyao.

Mavunde alitaja shughuli ambazo vijana hao wamekuwa wakishiriki mara wanapopata mikopo hiyo kuwa ni uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, kilimo, ufugaji pamoja usindikaji wa mazao.

Aidha amesema kuwa shughuli hizo zimewafanya vijana kuachana na utegemezi na badala yake kutumia muda wao mwingi katika kuzalisha na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Nchi.

Vile vile amesema kwamba, vipo vikundi ambavyo kupitia mfuko huo vimekuwa kielelezo cha dhati katika kubadili mtizamo wa  vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao.

Alivitaja vikundi hivyo kuwa ni kikundi cha Thyroid Group kutokana Halmashauri ya Chunya ambacho kinasambaza Taa za Solar Vijijini, kikundi cha Miranaco Group ambacho kinamiliki duka kubwa la dawa za Binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, kikundi cha Maswa Family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.

Aidha, ili kuboresha mfuko huo Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za kiutendaji zinazojitokeza.


Hata hivyo, katika mwaka huu wa fedha Serikali inapitia upya mwongozo wa utoaji fedha kupitia mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana ambao  ulioanzishwa mwaka 2013 ili kuwawezesha vijana wengi kuanzisha viwandaa vidogo vidogo katika kuendana na Sera ya Nchi ya kwenda kwenye Uchumi wa Viwanda.

No comments:

Post a Comment