Tuesday 7 February 2017

SERIKALI KUPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA POMBE AINA YA VIROBA NCHINI



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangala 

Serikali inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe za bei rahisi maarufu kama “Viroba” Nchini, ndani ya miezi mitatu ijayo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangala ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia  kilevi hicho kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi pamoja na Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2016/17.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa baada ya miezi mitatu kilevi hicho kitapigwa marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya yote ya uingizaji wa kilevi hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa na vijana wengi, hivyo kuharibu nguvu kazi ya Taifa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko amesema kwamba pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.

“Katika kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na tumezika vijana wanne ambao wamefariki kutokana na matumizi ya viroba. Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za pombe hiyo ili tuweze kujadili na kuona namna gani  ya kuliokoa Taifa hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya pombe hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia ongezeko la vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.


Aidha amesema kuwa hali hiyo inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Hivyo Kamati imeishauri Serikali kufungia kabisa uzalishaji na uuzwaji wa pombe hizo za viroba ili kulinusuru Taifa.

No comments:

Post a Comment