Thursday 2 February 2017

TANZANIA, MAKAO MAKUU YA LUGHA YA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Mosses Nnauye.

Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili kuwa Tanzania ambayo yatakuwepo Zanzibar.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya jitihada mbalimbali ambazo Tanzania inazichukua katika kukuza Lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Kimataifa.

Nape amesema kuwa maamuzi hayo ya kuifanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili yametokana na Tanzania kuzalisha walimu wengi wa Kiswahili ambao wanatumika katika ngazi mbalimbali za elimu ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Anastazia Wambura amesema kuwa Wizara hiyo kwa sasa inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa mawakala wa kulinda Lugha ya Kiswahili ambapo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na wadau wa Kiswahili limeendelea kuendesha semina, warsha, makongamano na kutoa elimu inayohusu matumizi fasaha ya Lugha ya Kiswahili.

Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa Waandishi wa Habari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Lugha  hiyo inaendelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya Lugha hiyo katika majukumu yao ya kila siku.

“Kutumia zana kama vile Kamusi na vitabu vya miongozo ya uandishi pamoja na kuhudhuria makongamano ya Kitaifa na ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili inasaidia kuongeza ujuzi na uweledi wa  Lugha ya Kiswahili, kujua istilahi za kisayansi na kiteknolojia na hivyo kuandika na kutangaza kazi bora na zenye maudhui lengwa kwa jamii na kuepuka upotoshaji wa maneno ya Kiswahili usio wa lazima,” alifafanua Anastazia Wambura.

Hata hivyo Wizara hiyo iko katika maandalizi ya Sera ya Lugha ambayo itabainisha majukumu ya Vyombo vya Habari katika matumizi na uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.



No comments:

Post a Comment