Thursday 19 April 2018

WATENDAJI KAMATENI WATORO NA WAZAZI WAO” - DC KAPUFI



Mkuu wa wilaya ya Geita  Mwalimu Herman  Kapufi amekutana na watendaji wa mitaa,vijiji, kata,elimu na afya kutoka Halmashauri za wilaya na Mji Geita kuwapa maagizo ya kukabiliana na tatizo la  utoro sugu na rejareja kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa.
Aidha amewataka watendaji hao kutoa taarifa sahihi na haraka kwa uongozi wa wilaya kwa familia zote ambazo watoto wametoroka shule na kwenda kufanya shughuli  mbalimbali za majumbani, migodini, uvuvi  na wale ambao wameozeshwa na familia zao.

Pia hakusita kuwaonya watendaji  ambao wamekua wakipokea kesi  za wanafunzi  kupewa mimba na baadhi ya watu maarufu vijijini kutofikisha taarifa  kwa uongozi wa wilaya na pia kawakemea viongozi wa  kisiasa ambao huwasaidia watuhumiwa wa utoro na mimba  kutochukuliwa hatua.

“Msibague mtu katika ukamataji huo,  kumekua na tabia ya wanyonge kuonewa katika matukio mbalimbali nawaomba hata wenye nguvu kama wametenda makosa  wakamatwe na wafikishwe mahakamani.”alisema DC  Kapufi.

Vikao hivi ni moja ya mkakati wa Mkuu wa wilaya ya Geita kuwapa maagizo watendaji wote wa serikali kuhakikisha wanaondoa tatizo la utoro na mimba mashuleni  kwani Wilaya ya Geita inashika nafasi ya pili kulinganisha na wilaya zingine Mkoani hapa..


No comments:

Post a Comment