Wednesday 25 April 2018

WANANCHI WAJITOLEA KUJENGA SHULE WILAYANI BARIADI MKOANI SIMIYU


Wananchi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wakijitolea kuchimba Msingi wa ujenzi wa vyumba 40 vya madarasa ili kuipandisha hadhi shule ya sekondari Simiyu iliyoko mjini Bariadi (Picha zote na Costantine Mathias).



Wananchi katika Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu, wamejitokeza kwa wingi kujitolea kuchangia nguvu kazi ili kuipandisha hadhi shule ya Sekondari Simiyu ili iweze kuwa shule ya vipaji maalumu.

Aidha wameitika wito wa Serikali ya Mkoa huo, wa kuchangia nguvukazi kwa kuanza kuchimba msingi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi 40 na mabweni 15 katika shule hiyo

’Tumekuja kujitolea nguvukazi kujenga shule hii ambayo tayari ilikuwepo japo inaonekana kuwa na sura ya shule za kata wakati inabeba jina la mkoa…shule hii wanasoma watoto wetu ni lazima tuijenge na watoto wapate elimu bora kwa maisha yao ya baadae’’ Alisema Yohana Kibusi Mkazi wa Mjini Bariadi.

Diwani wa kata ya Malambo Kulwa Kitebo alisema Simiyu sekondari ni shule inayobeba jina la mkoa, lakini hadhi yake ni ndogo sana ni vema wananchi wakajitolea kuijenga ili iwe katika kiwango kizuri kimiundombinu.

Alisema yuko bega kwa bega na wananchi kuhakikisha shule hiyo inajengwa, huku akiwataka wananchi kuendelea kujitolea nguvukazi kukamilisha ujenzi huo.

Akishiriki ujenzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema ujenzi huo ukikamilika itakuwa ni moja ya shule bora pekee inayowakilisha mkoa, yenye vymba vya madarasa 40 na mabweni 10.

Aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kushiriki ujenzi huo ambao wamejitokeza bila kulazimishwa ambo walikuja kushiriki ujenzi huo kwa hiari yao.

‘’Niwashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki ujenzi huo, hawajalazishwa na mtu, wamekuja kwa hiari yao…Rais anataka watu wajiletee maendeleo kwa kufanya kazi, wameguswa na uamuzi wa Serikali ya Mkoa huu, chini ya Uongozi wa Mtaka, kwamba kwa sasa Mkoa utakuwa na shule bora itakayo kuwa inachukua wanafunzi wa vipaji maalum’’ Alisema Kiswaga.

 Aliongeza shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 na kwamba Mkoa wa Simiyu utakuwa katika ramani ya Mikoa yenye shule bora.

Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka alisema Mkoa utajenga shule ya Mkoa Mjini Bariadi (Makao Makuu ya mkoa) ambayo itatambulika kama Shule ya Sekondari Simiyu na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 huku ikiwa na miundombinu muhimu kama maabara, vyumba vya kompyuta na mkongo wa Taifa.

Pia alisema pamoja na kujenga Shule hiyo ya Mkoa, Serikali imedhamiria kushirikiana na wananchi kujenga shule mbili maalumu kwa ajili ya wasichana na wavulana (Simiyu Girls na Simiyu Boy's) ambazo zitabeba taswira ya Mkoa na kutambulisha Mkoa huo tofauti na ilivyo sasa ambapo shule nyingi zilizopo katika Makao makuu ya Mkoa ni za Kata.

Shule ya Simiyu Sekondari kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 521 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, vyumba 10 vya madarasa vinavyotumika, vyoo matundu 6, maabara vumba vitatu, na haina jengo la utawala.




No comments:

Post a Comment