Thursday 12 April 2018

WANUFAIKA WA TASAF WALIMA EKARI 8712 ZA PAMBA MKOANI SIMIYU


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi wa mkoa huo wakati alipofungua kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi wa Mkoa huo juu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.

K
atibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na viongozi wa mkoa huo katika kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi wa Mkoa huo juu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.


Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu, Ndg. Nyasilu Ndulu akiwasilisha Taarifa ya Utekelzaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo, katika kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi wa Mkoa huo juu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.


Bw. Fariji Mishael mtaalamu wa ufuatiliaji wa tathmini kutoka Ofisi ya TASAF Makao  makuu akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, katika kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi hao juu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.


Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka katika cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi wa Mkoa huo juu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.


Kaya 6120 sawa na asilimia 52 ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu zimewezeshwa kulima pamba ekari 8712 katika Msimu wa mwaka 2017/2018 kwa kutumia fedha za uhawilishaji.

Hayo yalibainishwa na  Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu Bw. Nyasilu Ndulu wakati wa   kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi juu ya mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.

Nyasilu amesema pamoja na kulima pamba walengwa wa mpango huo katika Wilaya ya Bariadi na wilaya nyingine Mkoani Simiyu, kupitia fedha za uhawilishaji (wanazopewa) wamefanikiwa kujenga nyumba, kufuga, kuanzisha biashara ndogo ndogo na kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).

Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa zoezi la uhawilishaji chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini awamu ya tatu mwaka 2015 hadi sasa,  tayari awamu 17  za malipo zimekwisha fanyika kwa walengwa 37, 533 na jumla ya shilingi bilioni 28.9 zimelipwa kwa wahusika.

Amesema  fedha hizo zimejumuisha ruzuku za aina mbili ikiwa ni ruzuku ya msingi na ile itokanayo na utimizaji wa mashati ya Afya na Elimu ambapo watoto 39,068 sawa na asilimia 90.3 wameweza kupata mahitaji muhimu ya shule na kukuhudhuria shuleni na watoto 51, 280 sawa na asilimia 93.1 wamepata mahitaji ya kliniki na kupelekwa kliniki.

“Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeweza kuwasaidia walengwa kujikwamua kutoka kwenye umaskini, wapo walioanzisha biashara, wanaolima, wanaofuga, waliojenga nyumba bora; kwa kutumia fedha hizi wanazopewa wapo ambao watoto walikuwa hawahudhurii shuleni na kliniki lakini sasa hivi mahudhurio mazuri” Alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka awali akifungua kikao amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata walengwa, wanufaika wote waliofanya mambo  ya maendeleo ni vema wakawa mfano kwa wenzao huku akiwataka wale walioshindwa kuondolewa kwenye mpango huo.

Aidha, Mtaka  aliwataka  walengwa wote wa mpango kuendana na malengo ya nchi ya kuelekea kwenye Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 badala ya kuwaza kuendelea kubaki katika mpango huo.

“Mtazamo wangu mimi ni vizuri wanufaika wa TASAF waendane na Mpango wa Nchi, tunaposema tunataka kwenda kwenye Uchumi wa Kati kufikia mwaka 2025 wanufaika wa TASAF wanapaswa kujindaa kwenda kwenye uchumi wa kati, ili badala ya watu kutaka tu kuingia kwenye mpango,  tupate watu wanaotaka kutoka baada ya kupiga hatua na kutoka kwenye umaskini waliokuwa nao mwanzo” alifafanua Mtaka

Nae Bw. Fariji Mishael mtaalamu wa ufuatiliaji wa tathmini kutoka Ofisi ya TASAF Makao  makuu aliupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza mpango huo vizuri na kuomba wataalamu kuwasaidia walengwa walio kwenye maeneo yao katika  kuwashauri namna bora ya kuendesha miradi waliyoianzisha ili iwe endelevu na iweze kuwasaidia kiuchumi.

No comments:

Post a Comment