Friday 13 May 2016

SERIKALI YAPATA BILIONI 1.71 KUTOKANA NA MAONESHO YA VITO JIJINI ARUSHA.



TATHMINI YA MAONESHO YA TANO YA  KIMATAIFA YA MADINI YA VITO YALIYOFANYIKA JIJINI ARUSHA, HOTELI YA MOUNT MERU TAREHE 19 HADI 21 APRILI, 2016

Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa madini Tanzania (TAMIDA) iliendesha Maonesho ya tano ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika Jijini Arusha katika Hoteli ya Mount Meru kuanzia tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016. Maonesho haya  hufanyika kila mwaka Jijini Arusha  na hukutanisha washiriki mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wachimbaji, Wafanyabiashara wa madini ya vito wa ndani na  nje, wanunuzi wa madini wa ndani na nje, na wataalam mbalimbali wenye uzoefu wa shughuli za madini  ya vito.   

Maonesho hayo yalihudhuriwa na washiriki 813 kutoka katika nchi 26 duniani ambazo ni Tanzania  Marekani, Sri Lanka, India, Kenya, China, Ujerumani, Namibia, Australia, Austria, Israel, Italia, Uingereza, Hong Kong, Switzerland, Zambia, Madagascar, Afrika Kusini, Msumbiji, Urusi, Cameruni, Canada, Malawi, Sudani, Malta, na Thailand). Aidha, wanunuzi (buyers) wa madini walikuwa 353, Walioshiriki kuonesha madini kwenye mabanda (Exhibitors) 300, na wageni mbalimbali 160.

Lengo kubwa la Maonesho haya ni kama ifuatavyo: kufanya Arusha kuwa kitovu cha madini ya vito katika Afrika ili hatimaye iwe ni kitovu cha biashara ya madini hayo; fursa ya masoko kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa mdini ya vito nchini; na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito hapa nchini.

Katika maonesho hayo, madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.5, sawa na Shilingi Bilioni 9.9 yaliuzwa.
Serikali ilipata jumla ya Shilingi bilioni 1.71, ambapo Shilingi bilioni 1.3 zilitokana na mnada wa madini yaliyokamatwa na kutaifishwa na Serikali, Shilingi milioni 388 zilitokana na mrabaha uliolipwa kutokana na madini yaliyonunuliwa, na Shilingi milioni 26 zilitokana na vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi.

Manufaa mengine yaliyopatikana wakati wa maonesho ni pamoja na wageni kuingiza fedha za kigeni hapa nchini ambazo hutumika kwa ajili ya malazi, usafiri, chakula na kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii hapa nchini.

Ili kuweka utaratibu utakaodhibiti shughuli za madini ya vito  hususani tanzanite, Serikali inakusudia kuanzisha minada ya ndani mbali na mnada unaofanyika wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Vito Jijini Arusha. Minada hiyo itatoa fursa kwa wafanyabishara wa ndani kununua madini kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani madini hayo na kutengeneza vidani mbalimbali.  

Ili kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito nchini, Serikali inakusudia kuimarisha Kituo cha Jimolojia kilichoko Arusha (Tanzania Gemmological Centre -TGC) ili kufundisha na kuzalisha vijana wa Kitanzania wa kutosha wenye ujuzi wa kusanifu na kung’arisha madini ya vito. Tayari vijana 29 wameshapata mafunzo ya miezi 6 ya ukataji wa madini ya vito kutoka kwenye kituo hicho tangu 2014. Wanafunzi wengine 18 wanaendelea na mafunzo ya miezi 6 yaliyoanza mwezi Machi, 2016.

Aidha, upo mpango wa kuanzisha EPZ eneo la Merelani ambapo ni karibu na machimbo ya tanzanite kwa lengo la kupata eneo maalum ambapo shughuli za biashara ya madini na uongezaji thamani madini ya tanzanite zitafanyika kwa uhuru na wazi. Pamoja na juhudi zote hizo, Serikali itaendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini mbalimbali nje ya nchi ikiwemo Tanzanite kwenye viwanja vya ndege na kwenye migodi ambapo madini yanazalishwa.   

Wito wa Serikali ni kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuzingatia sheria zilizopo wakati wa kufanya shughuli zao.
Imetolewa na;

KAIMU KAMISHNA WA MADINI
MHANDISI ALLY SAMAJE

Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ally Samaje akieleza kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu Tathmini ya maonesho ya tano ya kimataifa ya madini ya vito yaliyofanyika Jijini Arusha mwezi April mwaka huu yaliyohudhuriwa na washiriki 813 kutoka nchi 26 duniani. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo Bi. Asteria Muhozya.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano huo


No comments:

Post a Comment