Monday 30 May 2016

WANANCHI MKOANI GEITA WALALAMIKIA KUTOZWA PESA ZA KUANDIKISHWA KATIKA DAFTARI LA MAKAZI

Wakazi  wa mtaa  wa  Uwanja  kata ya Nyankumbu mkoani Geita wamelalamikia suala la kutozwa pesa kwa ajili ya kuandikishwa katika daftari linalowatambulisha kuwa ni wakazi wa eneo hilo pindi wanapohamia katika mtaa  huo.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wanachi wa mtaa huo, walipokuwa wakizungumza na Storm habari mapema hii leo, ambapo wamesema kuwa wananchi wanaohamia katika eneo hilo wamekuwa wakitozwa viwango tofauti kwa kila mmoja jambo ambalo  limekuwa ni changamoto kubwa hususani kwa watu wenye vipato vya chini.

Kwa upande wake balozi wa kitongoji hicho bw, Alfred Kigongo amekiri kupokea pesa hizo ambapo amesema kuwa amekuwa akitoza pesa hizo kwa ajili ya kununulia mahitaji mbalimbali ikiwemo kalamu pamoja na daftari kwa ajili ya kuwaandika watu hao.

Hata hivyo Storm habari imezungumza na mwenyekiti wa mtaa huo bw, Joseph Msoma ambapo amekiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi  huku akiwataka mabalozi wote kuacha tabia hiyo mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Aidha mwenyekiti ametoa wito kwa wananchi wote wa mtaa huo kutoa taarifa katika ofisi yake pindi wanapata na jambo hilo ili mabalozi wote wanaojihusisha na kitendo hicho sheria  iweze kuchukua mkondo wake.


No comments:

Post a Comment