Friday 13 May 2016

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ATAKA HAKI ITENDEKE WAKATI WA KUTUMBUA MAJIPU

Wakati viongozi wakiendeleza kasi ya Rais John Magufuli ya utumbuaji wa majipu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wanaoiga kasi hiyo kutenda haki, ikiwamo kufuata taratibu na sheria.
Akizungumza kwenye maadhimisho Siku ya Wauguzi Duniani mkoani Geita jana, Samia aliwataka viongozi na wanasiasa kufuata taratibu za kazi, ikiwamo kutoa nafasi ya kujitetea kwa watumishi wanaotuhumiwa.

Alitoa kauli hiyo, baada ya wauguzi kulalamika kwenye hotuba yao kwamba kuna viongozi waliwatumbua wauguzi bila kuwatendea haki.

Hata hivyo, nakiomba Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), kuweka utaratibu wa kufuatilia maadili ya wauguzi na kuwachukulia hatua za kisheria, wale wote ambao wanakwenda kinyume na kiapo chao cha kazi,” alisema.

Rais wa Tanna, Magesa Paul alimuomba Makamu wa Rais kutembelea maeneo yao ya kazi, ili ajionee hali halisi ya wauguzi wanavyofanyakazi katika mazingira magumu, ikiwamo kukosa vitendea kazi na nyumba za kuishi.

Jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliwataka wauguzi kuhakikisha wanatii maadili ya kazi, bila hofu ya kupigiwa simu na baadhi ya viongozi wa Serikali waliozoea kutaka upendeleo wa huduma, kinyume na maadili yao.

Tunaomba wauguzi mkitendee haki kiapo chenu cha kazi, na mtumie siku hii muhimu kuutathmini utendaji wenu wa kazi katika kuwasaidia wananchi,” alisema.

Alisema Serikali inatambua changamoto za wauguzi, hivyo wasitumie matatizo yao katika kuwanyanyasa wagonjwa, bali wawasaidie na kuwaonyesha upendo.

Akisoma risala kwa niaba ya wauguzi wenzake, muuguzi wa Hospitali ya Temeke, John Mgonja alilaani tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kutumia madaraka kuvuruga utaratibu wa muda wa kuwaona wagonjwa.

Bila kujali muda uliowekwa wa kuwaona wagonjwa, baadhi ya viongozi hutaka kuingia kuwaona wagonjwa wao kutokana na madaraka waliyo nayo, bila kujali kuwa kufanya hivyo kunachelewesha huduma,” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Musa Wambura aliwaomba wauguzi kuhakikisha wanafanya kazi kwa umakini na weledi, ili kuepusha lawama kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment