Thursday 19 May 2016

BENKI YA MAENDELEO YA KILIOMO CHINI (TADB)YAJIPANGA KUWAKOMBOA WAKULIMA NCHINI

Kwa miaka kadhaa sasa kilimo kimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania hasa katika upatikanaji wa chakula, biashara ya mazao nje ya nchi, kusaidia upatiakaji wa malighafi za viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa Watanzania.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2015 Tanzania iliuza jumla ya tani 125,134 za mazao ya kilimo katika soko la nje ikiwemo tani 63,237 za mahindi, Ngano tani 42,538, Mpunga Tani 7,651 na Mihogo Tani 11,708.
Pamoja na kwamba zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania watagemea kilimo na kutoa zaidi ya asilimia 65 ya malighafi kwa ajili ya viwanda nchini, asilimia kubwa ya shughuli za kilimo zinafanywa na wakulima wadogo.

Hata hivyo pamoja na umuhimu na sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi, bado ukuaji wa sekta hiyo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kiwango kidogo cha uzalishaji, ukosefu wa mbinu na teknolojia za kisasa, matumizi madogo ya umwagiliaji, ukosefu wa mtaji na ukosefu wa mikopo kwa wakulima.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa ni jitihada za Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo nchini.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa benki hiyo Dkt. Jakaya Kikwete alisema kuwa Serikali imekuwa ikisaidia sekta ya kilimo kupitia ruzuku za pembejeo na mbolea na kwa sasa imeanzisha benki ili kero mbalimbali za wakulima zitatuliwe kwa wakati.

Pia Dkt. Kikwete aliwataka wakulima kutambua kuwa kilimo ni shughuli inayoweza kuwaletea kipato kikubwa, hivyo watutumie fursa zinazotolewa na Benki ya Kilimo katika kuendeleza sekta hiyo na kujiongezea zaidi kipato kwani ni wakati kwa wakulima kufanya shughuli hiyo kiutaalamu zaidi badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea.

Mbali na kutekeleza sera ya Serikali kuhusu upatikanaji wa fedha za kuendeleza kilimo, pia benki ya kilimo imepanga kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula utakaokuwa endelevu na kusaidia kuleta mapinduzi ya kilimo ili kuwatoa watanzania katika kilimo cha mazoea kwenda katika kilimo cha kibiashara.
Katika kutimiza lengo la kuanzishwa kwake Benki ya kilimo imetoa elimu kwa wakulima ambapo vikundi 89 vyenye Wakulima 21,526 vilipatiwa elimu mkoani Iringa, kufanya tafiti mbalimbali kwenye sekta ya kilimo, kuwajengea uwezo wakulima hasa vijana katika kuanzisha miradi ya kilimo ili pale watakopewa mikopo waweze kuitumia vizuri na kuwaletea faida katika shughuli zao.
Benki imejipanga kutoa mikopo ya mudamfupi, (Hadi Miaka 2); muda wa kati (zaidi ya miaka 2 hadimiaka 5); na muda mrefu (zaidi ya miaka 5 hadimiaka 15) kwa Wakulima wadogowadogo, wa kati na wakubwa ili kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugajinyuki).

Akiongea na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo  Bw. Thomas Samkyi alisema Benki hiyo imejipanga kutoa mikopo ya  muda mfupi, wa kati na mrefu kwa riba nafuu (kati ya 7% hadi 12%) kwa kupitia muungano wa vikundi vya Wakulima wadogo wadogo, benki za maendeleo ya jamii, vyama vya kuweka na kukopa, taasisi ndogo za fedha, vyama vya ushirika na taasisi au vyama vya wakulima.

Bw. Semkyi aliongeza kuwa benki hiyo imetoa mikopo kwa wakulima kwa kwa vikundi 8 vya wakulima wapatao 857 na sasa inashughulikia maombi ya mikopo kwa awamu nyingine yenye thamani ya Zaidi ya Sh Bilioni 40.

“Napenda kuwashauri wakulima wajiunge katika vikundi ili kuirahisishia benki kuwatambua na kutoa mikopo ya riba nafuu ya kati ya asilimia 7 hadi 12 ili waweze kuendesha shughuli zao za kilimo katika maeneo ya uzalishaji mazao, uvuvi na ufugaji hali itakayowawezesha kuwatoa katika kufanya kilimo cha mazoea na kwenda katika kilimo cha kibiashara” Alisema Bw. Semkyi.

Akifafanua kuhusu aina ya riba hasa kwa vikundi, Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa Benki ya Kilimo Bw.Robert Paschal alisema kuwa Riba yake ni asilimia saba hadi nane na wanaokopeshwa ni wakulima wadogo walio kwenye vikundi.

Alisema wakulima hao watapata mkopo kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora, kulima shamba na mahitaji mengine ya shamba ambapo marejesho ya mkopo huo ni mara baada ya mkulima kuvuna mazao.
Bw. Paschal aliongeza kuwa kama msimu wa mavuno haukuwa mzuri, labda mvua hazikunyesha na mkulima hawakupata mavuno, wakijiridhisha na ukweli wa hilo, mkopo unasogezwa msimu unaofuata.
Aidha Bw. Paschal alisema kuwa aina nyingine ya mkopo ni wa kati, unaotozwa kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitano na riba yake ni asilimia tisa hadi 10, na mkopo huo ni kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa vifaa vya kilimo na upanuzi wa mashamba.

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata baada ya kupata mkopo kutoka TADB, kiongozi wa Chama cha Nzihi Mixed Crops kilichopo Mkoani Iringa Bw. Emmanuel Fungo anasema benki hiyo imewapatia mkopo wa shilingi Milioni 222 ambao umewasaidia  sana kwa sababu wameupata kwa muda walioutarajia na bila masharti magumu tofauti na taasisi nyingine zinazolazimu kuhamishia akaunti yako kwenye taasisi hiyo.

Anasema sanjari na kuwapatia mkopo huo pia TADB imewatafutia mteja wa mazao (Mahindi) watakayozalisha hivyo wana uhakika watauza mazao na kuweza kulipa mkopo na kubaki na mazao ya ziada.
Rai yangu kwa wakulima ambao mara nyingi wamekuwa wakilalamikia uhaba wa rasilimali fedha katika kuendeleza shughuli zao za kilimo ni kutumia fursa inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
Alisema benki hiyo imejiwekea malengo katika utoaji mikopo ya uongezaji wa thamani katika shughuli za kilimo na kuwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika wa mazao wakati wa mavuno.


No comments:

Post a Comment