Tuesday 17 May 2016

WANANCHI WAISHIO KARIBU NA MGODI WA DHAHABU WA GEITA(GGM) BADO HAWANA UELEWA JUU YA FAIDA ZIPATIKANAZO NA MGODI HUO


Imebainika kuwa jamii kubwa inayoishi karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM),  hususani maeneo ya vijijini  bado hawajawa na uelewa wa kutosha  juu ya faida ambazo zinatolewa na  mgodi huo, ambao umekuwa ukishirikiana na  Serikali  katika kutatua  changamoto mbalimbali  huku wananchi wakiaminishwa kuwa  hakuna faida  yoyote inayotokana na mgodi huo.

Kutokana na kuwepo kwa mawazo hayo  GGM  kwa kushirikiana na  Halmashauri ya Wilaya ya Geita  wamefanya  semina  kwa  wanafunzi  wa shule za sekondari  huku lengo ikiwa  ni kuwajengea   uelewa kuhusiana  na Mgodi huo  ili  wawe mabalozi wazuri katika jamii  inayouzunguka mgodi huo.

Kufuatia Semina hiyo Wanafunzi wamejifunza mambo  mbalimbali, huku wakipata fursa  ya  kuuliza maswali ambayo yalikuwa yakiwasumbua  kwa  muda mrefu na miongoni mwa mambo waliyoyauliza ni pamoja na suala la ajira Mgodini ambapo Meneja Mahusiano  wa Mgodi Joseph Mangilima  na  Afisa utamaduni wa halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw.Mfungo Phares wakawa  na  majibu

Meneja mahusiano wa GGM, Joseph Mangilima amesema kuwa katika semina hiyo kuna  maombi ambayo yameombwa na wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuombwa kujenga  mabweni kwa  shule  zilizopo  vijijini  hivyo kutokana na maombi hayo wataangalia ni wapi serikali imekwama ili wao waweze kuongezea.

Kwa upande wao wanafunzi wamesema wameelewa namna ggm  inavyosaidia jamii na kuwa na mchango mkubwa kwa serikali na wamefarijika na mafunzo waliyopata, huku baadhi ya wanafunzi  wasichana wakitamba  kukabiliana na masomo  ya  sayansi hii ni kufuatia  hamasa waliyopewa.



No comments:

Post a Comment