Sunday, 15 October 2017

AWESO; AAGIZA WAKANDARASI WASIOKAMILSHA KAZI WAKAMATWE.

Naibu Waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akiangalia mtambo wa kuvuta maji kwenda kwenye chujuo katika bwawa la New Sola (Zanzui).

Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akionyeshwa jinsi chanzo cha maji katika bwawa la New Sola (Zanzui) katika mji wa maswa kilivyokauka na kusababisha ukosefu wa maji.

Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akionyeshwa jinsi chanzo cha maji katika bwawa la New Sola (Zanzui) katika mji wa maswa kilivyokauka na kusababisha ukosefu wa maji.


NA COSTANTINE MATHIAS, SIMIYU.


Siku  chache baada ya Rais Dk John Magufuli kuwateuwa na kuwaapisha Mawaziri na Manaibu wao alipofanya mabadiliko madogo katika Baraza, Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji,Jumaa Aweso amefanya ziara mkoani Simiyu ya kukagua tatizo la maji wilayani Maswa.


Naibu waziri huyo ameaagiza wakandarasi wote waliolipwa fedha na serikali kwa ajili ya kujenga miundo mbinu ya maji kote nchini  na kushindwa kukamilisha kwa wakati  wachukuliwe hatua na ikibidi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.


Hayo aliyasema jana mjini Maswa mkoani Simiyu alipofanya ziara ya siku moja  mara baada ya kutembelea Mradi wa ujenzi wa chujio la maji ya kunywa ulioko katika bwawa la new Sola katika kijiji cha zanzui.


Akizungumza jana mjini Maswa na wafanyakazi wa kampuni za PET Cooperation na Jossam & Company Ltd zote za mjini Kahama mkoani Shinyanga zinazojenga mradi huo, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha kazi hiyo kutokamilika kwa wakati licha ya serikali kuwalipa fedha zote.


Alisema kuwa kitendo cha Kampuni hizo kulipwa fedha na serikali na kushindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati hakivuliki na atachukua hatua kali dhidi ya kampuni zote hapa nchini zitakazoendelea kufanya kazi kwa mazoea.


“Haiwezekani mkandarasi amelipwa kiasi chote cha fedha  na serikali za kutekeleza mradi halafu wanashindwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa visingizio mbalimbali hata kama una mapembe marefu mimi kwa umri wangu huu mdogo lakini nimepewa madaraka nitakufuata huko huko ulipo na kuyakata mapembe hayo,”alisema.



February mwaka huu, Aliyekuwa  Waziri wa Maji na Umwagiliaji Gerson Lwenge alimpa siku 132 mkandarasi huyo,  kuhakikisha anakamilisha kazi yake na kumtahadharisha kuwa endapo hatakamilisha kwa mujibu wa mkataba aliopewa atakuwa hana sifa ya kufanya kazi nchini.


‘’muda ambao wewe mkandarasi tumekuongezea wa ziada ili kukamilisha kazi hii, tunakuomba ukamilishe kwa wakati vinginevyo hatutakuonea aibu kukushughulikia…ifikapo juni 30 ujenzi wa chujio hili uwe umekamilika”Alisema Waziri Lwenge.


Viongozi wengi wa serikali wamekuwa wakifika katika mradi huo na kutoa maagizo kadhaa lakini hakuna utekelezaji wowote unaofanyika, na badala yake wananchi kuendelea kuteseka na adha ya kukosa maji.

No comments:

Post a Comment