Muswada wa Sheria ya Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017
inatarajia kuleta mabadiliko makubwa ndani ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na
kuliondoa shirika hilo katika hali ya ufilisi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na
Mawasiliano Elias John Kwandikwa wakati wa majadiliano ya muswada huo baina ya
wizara hiyo na Kamati ya Bunge ya Miundombinu, leo mjini Dodoma.
“Muswada wa Sheria ya Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017
itaiondoa TTCL katika usajili wa muundo wa kampuni na kurejeshwa kwenye
Mashirika ya Umma ambapo kwa asilimia 100 litakuwa chini ya Serikali,” alisema Kwandikwa.
Ameendelea kwa kusema kuwa baada ya kupita kwa sheria hiyo
mabadiliko makubwa yatafanyika ndani ya shirika hilo ambapo Waziri mwenye
dhamana ataanza kutoa maagizo na maelekezo kwa shirika hilo ikiwa ni
maelekezo ya jumla pamoja na utendaji kazi wa shirika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Norman Sigalla
amesema, kamati imeshauri sheria iseme uzoefu wa Mwenyekiti wa bodi pamoja na wajumbe
wake katika kufanya biashara.
“Kwa kuwa shirika sasa linakuwa la kibiashara hivyo ni vyema
mwenyekiti pamoja na wajumbe wa bodi wakawa na uzoefu wa kufanya biashara ili
waweze kuliongoza shirika hilo kwa ufasaha,” alifafanua Prof. Sigalla.
Aidha kamati hiyo imeshauri Waziri mwenye dhamana ajikite katika
kuangalia utendaji kazi wa shirika pamoja na masuala ya mapato na kuiacha bodi
kufanya kazi yake pasipo kuingiliwa.
Vile vile imeshauri kuwa, mwenyekiti wa bodi, wajumbe na
wakurugenzi wa shirika hilo waadhibiwe kutokana na utendaji wao wa kazi na si
vinginevyo.
Muswada wa Sheria ya
Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017 utafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kupitiwa na kujadiliwa na Bunge lote. Bunge
litakapopitisha muswada huo utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kutiwa saini na
kuanza kutumika kama sheria.
No comments:
Post a Comment