Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mabaraza
ya Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu Mkoani Simiyu
yameridhia Halmashauri hizo kukopa shilingi bilioni 17.1 kutoka Benki ya
Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa ajili ya kutekeleza Miradi mikubwa miwili ya
Maendeleo.
Maridhiano
hayo yamefikiwa katika Vikao vya dharura vya mabaraza ya madiwani
vilivyofanyika kwa nyakati tofauti, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepanga
kukopa shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo cha
Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili (eneo la ekari 2050) na Meatu shilingi bilioni 6.4 kwa ajili ya
upanuzi wa kiwanda cha maziwa(MEATU MILK).
Akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Mpango wa
Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani Busega, Afisa Mipango wa Wilaya hiyo Josephat
Joseph, amesema hadi sasa kazi za upimaji wa mashamba na njia ya kupita bomba
la maji, kupima udongo, kusanifu mfereji mkuu kwenye chanzo, sehemu ya
kuchukulia maji, nyumba za pampu, mifereji ya kuingiza na kutolea maji,kuandaa
michoro na gharama za mradi zimeshakamilika.
Aidha, amesema
katika utekelezaji wa mradi huu Halmashauri ndiyo msimamizi mkuu wa mradi na itajenga
miundombinu yote ya umwagiliaji, hivyo itaingia makubaliano na wakulima wa
Mwamanyili kupitia umoja wao watakaounda katika kutekeleza shughuli za mradi.
Nao wakulima wa
Bonde la Mwamanyili wamesema wameupokea mradi huo kwa mikono miwili na kwa sasa
wamesitisha shughuli zote za Kilimo katika bonde hilo, ili kupisha shughuli nyingine
za maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.
“ Tunawashukuru viongozi
wetu kwa kutusaidia kupata mkopo wa kutekeleza mradi huu naupokea kwa mikono
miwili tena natamani uanze haraka, sasa hivi hatutalima maeneo yetu tunapisha
wataalam waendelee na shughuli za maandalizi ya mradi ili wakikamilisha tu
tuanze ” alisema Joseph Mayala.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema kutekelezwa
kwa mradi huo, kutaiandikia historia wilaya ya BUSEGA kwa
kuwainua wananchi kiuchumi na kuondokana na aibu ya kuomba chakula cha msaada
Serikalini, ambapo amesisitiza kuwa utakuwa mradi wa pekee ambao mnyororo wake
wa thamani utaonekana kupitia mazao yatakayolimwa hususani mpunga.
Kwa upande wa
Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Meatu, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza amesema kuelekea upanuzi wa
kiwanda hicho, Halmashauri imekusudia kuongeza idadi ya wafugaji wanaopeleka
maziwa kiwandani kutoka 45 wa sasa na kufikia wafugaji 400 wakubwa ambao wanafuga
ng’ombe wa kisasa.
Mikakati mingine
ni kununua mtambo mpya wa kuchakata maziwa wenye uwezo wa kuchakata lita elfu
15,000 kwa siku, kununua Mitamba 1000 na kuandaa shamba la malisho lenye
miundombinu muhimu pamoja na kuongeza soko la MEATU MILK kwa kuingia mikataba
na mawakala na kuweka maduka katika baadhi ya miji mikubwa.
Wafugaji wa
Wilaya ya Meatu wamesema wameupokea mradi wa upanuzi wa kiwanda cha maziwa
wilayani humo kwa furaha, kwani utawasaidia kuongeza upatikanaji wa soko la
uhakika la maziwa.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe.Pius Machungwa ametoa wito kwa wafugaji kukubali
kubadilika na kuanza kufuga kisasa kulingana na jinsi wanavyoshauriwa na
wataalam ili kuongeza tija
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali
mkoani humo imejipanga kutafuta majawabu
ya changamoto za wafugaji kwa kuwasaidia kufuga kisasa, ikiwa ni pamoja na
kuwashauri kupima maeneo yao na kuyawekea miundombinu muhimu kama mabwawa,
visima, majosho na mashamba ya malisho.
“Kiwanda mnachokihitaji
hapa kitatumia lita 15,000 kwa siku, mnapaswa kuweka mikakati mizuri ya ng’ombe
wenu ili muwe na uhakika wa maziwa, nayazungumza haya ili kila mmoja aone
umuhimu wa kiwanda; tuwasaidie wafugaji wafuge kisasa na kwa tija” alisema
Mtaka
Halmashauri ya
Wilaya ya Busega na Meatu zinatarajia kupata Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya
Kilimo ambayo imekubali kutoa mikopo hiyo ili kuunga mkono juhudi za Viongozi
na wananchi wa mkoa wa Simiyu katika kuleta maendeleo.
No comments:
Post a Comment