Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Nyalandu ameandika Ujumbe huu kama unavyosomeka hapo chini.
NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo,
Oktoba 30, 2017.
HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job
Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida
Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne
mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.
AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutoridhishwa kwangu na mwenendo
wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za Kibinadamu,
ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na
kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na
Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa
Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.
VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna
namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa
wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama
ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa
madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu
kwajili ya Watu.
MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia
kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na
Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa,
kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa
kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama
ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila
kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya
miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi
kama yalivyokuwa maono ya Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.
HIVYOBASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na
haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na
nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,
basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na
CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi
nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.
VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini
kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua
ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki
nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala
uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, SOTE kama TAIFA
tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu
kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa
watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila
yote nchini uimarike. Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini
tubaki kama ndugu, na TAIFA lililo imara na nchi yenye ADILI.
#MunguIbarikiTanzania.
Lazaro S. Nyalandu.
No comments:
Post a Comment