Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt John Magufuli
na Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ni miongoni mwa viongozi
wanaotarajiwa kuhudhuria katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa Kenya,
Uhuru Kenyatta.
Kamati ya maandalizi ya sherehe hizo inayoongozwa na Katibu
Kiongozi, Joseph Kinyua imebainisha kuwa imeandaa orodha ya majina ya viongozi
wa kimataifa kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la kihistoria la uapisho wa
Kenyatta endapo ushindi wa Kenyatta hautopingwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, sherehe za uapisho hufanyika
siku 14, baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa ili kutoa fursa kwa chama
chochote kinachotaka kupinga matokeo kufanya hivyo.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kualikwa katika sherehe hizo
wakiwemo wakuu wa nchi ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Uganda
Yoweri Museveni, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na Rais wa Nigeria Muhammadu
Buhari. Wengine ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa
Uingereza Theresa May.
Aidha, katika orodha hiyo pia yupo Rais wa Liberia, Ellen
Johnson Sirleaf, mfanyabiashara tajiri namba moja Afrika Aliko Dangote,
Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Aga Khan, Waziri Mkuu mstaafu wa Italia,
Matteo Renzi na Rais Xi Jinping wa China.
“Tupo kwenye
maandalizi ya sherehe za uapisho wa Rais wakati tukisubiria hatua za kikatiba
kukamilika. Orodha hii ni ya marafiki wa Kenyatta, viongozi wa Afrika na
viongozi wengine wa kimataifa, tunaotarajia kuwaalika”, amesema mmoja wa
wanakamati hiyo ya maandalizi.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi Kenya, Wafula
Chebukati mwishoni mwa wiki alimtangaza rasmi Rais Kenyatta na Naibu wake,
William Ruto kuwa washindi katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini
humo.
No comments:
Post a Comment