Thursday, 24 August 2017

BINTI AISHI KWA KUFUNGWA KAMBA MIGUUNI KWA MIAKA MITANO MKOANI GEITA




Lyaki Juma akiwa kwenye mazingira ya nyumbani kwao.



Binti Lyaki Juma akiwa amefungwa na kamba miguuni kwake ili hastoroke Nyumbani kwao. 

Msichana mwenye umri wa miaka 26 mkazi wa mtaa wa nyakato Kata ya Ihanamilo kwenye Halmashauri ya mji wa Geita anadaiwa kufungwa kamba kwenye miguu yake kwa zaidi ya miaka mitano kutokana na tatizo la utindio wa ubongo.
Msichana huyo anayejulikana kwa Jina la Lyaki Juma ambaye anaishi kwa kufungwa kamba miguuni kwa madai kuwa amekuwa akitoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana hali inayompa wakati mgumu mama yake mzazi kwa kumtafuta licha ya hatari anazokutana nazo ikiwemo kubakwa na watu wenye nia ovu.

Mama Mzazi wa Msichana huyo Mwakami Shingashinga amezungumza  na Maduka online ambapo  amesema mwanaye alimzaa akiwa na akili timamu lakini alianza kubadilika alipofikisha umri miaka saba baada ya kuanza kuugua mara kwa mara.

 “Mwanangu alianza kupata tatizo hili baada ya kufikisha miaka saba alikuwa akikimbia na kwenda kusikojulikana na hata nilipomtafuta nilikuwa nikimkuta yupo mbali na eneo la nyumbani muda mwingine namkuta mlimani”Alisema Mwakami.

  Jirani wa karibu wa Familia hiyo Bi Verediana Joseph amesema kuwa mama huyo ana shida kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumhudumia mtoto huyo kwani kipato chake cha kifedha ni kidogo.

“Kiukweli hali ya mama huyu inasikitisha sana kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha na hata hivyo kuna watu ambao hawana nia nzuri wamekuwa wakimbaka na kumfanyia kitendo cha kinyama binti yake pindi anapokuwa ametoka kikazi hivyo naweza kusema kuwa amekuwa akiishi kwa wasiwasi sana na muda mwingine anakosa amani kutokana na watu kushindwa kumuhurumia”Alisema Bi,Verediana.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato Charles Kulola ameelezea kuwa mtoto huyo ana baba yake Mzazi lakini amekuwa akimkana kuwa sio mwanawe.

“Baba yake anaitwa Juma yupo kabisa hapo mtaa jirani lakini jambo la kusikitisha ameendelea kumkana mtoto wake jambo ambalo sisi tunaona kuwa sio zuri kwani ukizaa mtoto mlemavu kuna sababu gani ya kumkataa jamani mbona watu wanakosa imani”Alisema Mwenyekiti.


No comments:

Post a Comment