Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango
amesema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi na itaendelea kushirikiana
nayo katika kuhakikisha azma ya Tanzania ya viwanda inafikiwa.
Dkt. Mpango alisema hayo Jijini Dar es Salaam leo
alipokuwa akizindua kitabu cha Safari ya Tanzania kuelekea katika Uchumi wa
Viwanda 2016- 2056, kilichoandikwa na watanzania wazalendo Bw. Ali Mufuruki, Gilman
Kasiga na Moremi Marwa.
‘’Kitabu hiki ni kama mkombozi kwa sisi watunga sera
kwani kitatusaidia katika kuyafanyia kazi mapendekezo ambayo yametolewa ili
kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana, nimewaelekeza pia Tume ya Mipango
na Idara ya sera katika Wizara ya Fedha kuchukua mapendekezo ambayo wataona
yataisaidia serikali katika kutekeleza azma yake ya kuendeleza viwanda’’alisema
Dkt. Mpango
Bw. Ali Mufuruki mmoja wa watunzi wa kitabu hicho
alisema wameamua kuunganisha mawazo yao pamoja na kutumia utaalamu na uzoefu
wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na uchumi ili kuisaidia serikali
kuweza kuondokana na uchumi unaotegemea kilimo na hatimaye kuwa nchi ya
viwanda.
‘’Kuna changamoto nyingi zinazozikabili nchi
zinazoendelea ikiwemo ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha kisasa, ukosefu wa
mitaji pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kutosha hivyo kwa kuwa azma ya Mh. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwa na nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda,
tukaona tumuunge mkono katika kutimiza ndoto hiyo kwa kuandika kitabu hiki’’
alisema Mufuruki.
Bw. Mufuruki alisema kuna mambo mengi mazuri ya
kulisaidia taifa ambayo yameainishwa katika kitabu hicho hivyo ni vyema
watanzania wa kawaida, wasomi, wachumi na hata wawekezaji wakakisoma ili kuona
kila mmoja katika nafasi yake anawezaje kuisaidia nchi kutoka hapa ilipo na
kufikia katika malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wake Bw.Gilman Kasiga ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Kampuni ya General Electric katika ukanda wa Afrika Mashariki,
alisema ni vyema Tanzania ikawekeza katika masomo kwa kutambua vipaumbele kama inavyofanya
nchi ya Ujerumani ambapo sio kila anayesoma ni lazima afikie ngazi ya shahada
ndipo aonekane anaweza kuleta mchango katika maendeleo.
Bw. Kasiga alisema asilimia 70 ya wanaomaliza shule
hapa nchini wanakimbilia kusoma shahada na kusahau kwamba kuna masomo mengine
katika ngazi za astashahada na cheti ambayo kama yakifundishwa kwa umakini na
kwa kuzingatia fani husika yanaweza kuzalisha wataalamu wengi ambao wataisaidia
nchi kupiga hatua kimaendeleo na pia wao kupata ajira kwa urahisi katika
viwanda.
Alisema elimu ya vyuo vikuu ni ya kuandaa wasimamizi
yaani mameneja na sio watendaji au wafanya kazi na mafundi hivyo ameshauri
mitaala ya vyuo iendane na ukuaji wa viwanda ili wataaalamu hao waweze kutumia
taaluma zao katika kulitumikia taifa.
No comments:
Post a Comment