Wednesday, 16 August 2017

MBIO ZA MWENGE WA UHURU ZAMALIZIKA MKOANI GEITA

Mkuu wa Wilaya ya Magu akipokea mwenge wa uhuru kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati wa makabidhiano ya kimkoa.


Mkuu wa wilaya ya Magu Hadija Nyembo akisoma taarifa na shughuli ambazo zitafanywa na mwenge wa uhuru kwenye Mkoa wa mwanza.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimemalizika Mkoani Geita huku kukionekana baadhi ya miradi ya serikali kuwa na mapungufu mengi kuliko ya watu au sekta binafsi ambayo imekuwa ikizinduliwa na kuwekewa Mawe ya Msingi.

Hayo yamebainishwa na Frederick Joseph Ndahani Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Wakati alipokuwa akitoa salamu za mwenge wa Uhuru Wilayani Geita, amesema kuwa miradi ya serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuliko ya binafsi na bado inakuwa na mapungufu ambayo yamekuwa yakisababisha miradi hiyo kutokuzinduliwa.

Ameendelea kuongeza kuwa tatizo kubwa ambalo linasababisha miradi ya serikali kuwa mibovu ni kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu na kujikuta wakitumia mwanya huo kujilimbikizia mali huku wakiacha miradi ya serikali ikiharibika kabla ya muda.

Akikabidhi mwenge wa Uhuru kwenye Mkoa wa Mwanza,Wilayani Sengerema,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo,Mkuu wa Wilaya ya Geita,MwL,Herman Kapufi ameelezea kuwa kati ya miradi sabini na mbili (72) ambayo imepitiwa na mbio za mwenge wa uhuru miradi miwili (2) haikufanyiwa kazi kutokana na kutokukidhi vigezo vya kuzinduliwa na kwamba yale makosa ambayo wameambiwa kurekebisha watahakikisha wanarekeshibisha.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini,Constantine Kanyasu amesema kuwa tatizo lipo kwenye usimamizi  kwa kumkabidhi mkandarasi bila ya kufuatilia Miradi husika na kumwamini kuwa anaweza kufanya bila ya kukosea kwenye swala la ujenzi.

Mwenge wa uhuru umemaliza kuzindua,kutembelea na kuweka mawe ya msingi Kwenye Halmashauri sita zilizopo Mkoani Geita na kukabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya  ya Magu  Bi,Khadija Nyembo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu Wilaya ya  Geita,Mwl Hermani Kapufi kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita makabidhiano ambayo yamefanyika kwenye Kijiji cha Nyamadoke,Jimbo la Buchosa Wilaya  ya Sengerema.

No comments:

Post a Comment