Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Makao Makuu ya TAKUKURU jijini Dsm alipofanya ziara leo Agosti 28
Rais Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Valentino MlowolaRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na
ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo tarehe 28 Agosti,
2017 alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa TAKUKURU katika ofisi za
makao makuu ya taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Kuna mambo mengi ya
hovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini madai ya Shilingi
Bilioni 48 ni hewa, tumebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, tumebaini kaya
masikini hewa 56,000 zilizopaswa kupata fedha TASAF, tumebaini wanafunzi hewa 5,850
waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwepo
mkataba na mengine mengi, haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona
mnachukua hatua stahiki” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema ana imani na TAKUKURU na amewataka
wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na
uadilifu mkubwa na kwamba Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.
Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amepokea masuala
mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa TAKUKURU na amewaahidi kuwa Serikali
itayafanyia kazi ili kuboresha maslahi yao na mazingira ya kazi.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Katibu
Mkuu Dkt. Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Valentino
Mlowola.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya
mazungumzo na viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa
ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’
Gorge Hydropower Project), ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa
(Standard Gauge) na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Katika Mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt.
Medard Matogolo Kalemani ametoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa
ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza kwa
ujenzi huo itatangazwa tarehe 30 Agosti, 2017.
Mhe. Rais Magufuli amesema fedha za kuanza kwa ujenzi wa mradi
huo mkubwa utakaozalisha Megawatts 2,100 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa
zipo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Agosti, 2017
No comments:
Post a Comment