Maeneo ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM)Shughuli
zikiendelea za uchimbaji madini ya dhahabu.
Familia ya kijana Shija Charles mwenye umri wa miaka 25 imegoma kumzika
ndugu yao huyo wanayedai kuwa amefariki baada ya kupigwa na walinzi wa
mgodi wa dhahabu wa GGM na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Tukio la kuuawa kwa kijana huyo limetokea juzi Majira ya saa moja usiku
wakati akiwa na wenzake wawili walipoingia kwenye mgodi huo kwa madai ya kwenda
kuchukua Mawe ambayo yanajulikana kwa jina la Magwangala.
Vijana walionusurika kwenye tukio hilo Filipo Enock na Shija Mashemba
wamesema waliingia kwenye eneo la mgodi kwenye eneo la Piti na wakati
wanateremka kwenye maeneo ya barabara ya mgodi walikutana na
walinzi na kwamba mwenzao alikamatwa wakati wakikimbia .
Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu alikokuwa akiishi kijana
aliyeuawa Bw Hassan Mshora Malima amesema baada ya kupata taarifa za kifo hicho
walifika kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mkoa wa Geita
na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha ya kupigwa.
Msemaji wa Familia ya kijana huyo Bw Kazimili Malole amesema hawako
tayari kuchukua mwili huo kwa ajili ya maziko hadi watakapopata ukweli wa kifo
chake.
“Sisi kama familia hatupo tayari kuchukua mwili wa marehemu
hadi pale uchunguzi utakapo fanyika kujua ndugu yetu ni kipi ambacho
kimepelekea kuondoa uhai wake na tunaomba serikali itusaidie kwa swala hili
tupate haki zetu za msingi”Alisema Kazimilia.
Meneja mahusiano ya jamii wa Mgodi huo Bw Manase Ndoroma amekanusha
taarifa za kupigwa kwa kijana huyo hadi kufariki na kwamba alianguka kwenye
shimo mgodini na kwamba viongozi wa jadi waliitwa kushuhudia tukio hilo.
“Mgodini ndani kuna mashimo ambayo huwa tunachimba na kuyaacha wazi watu
wamekuwa wakiingia kinyemela kwenye maeneo hayo ambayo ni hatarishi kwa maisha
yao na mwisho wa siku wengi huanguka na kupoteza maisha kutokana na maeneo hayo
kuwa na mwamba mkali,na sisi tumekwisha kusema kama kuna mwananchi anahitaji
kuja mgodini kwa ajili ya kuona shughuli za uchimbaji ni vyema
wakafuata utaratibu kuliko kuingia kinyemela kwani kuna maeneo ambayo ni
hatarishi”Alisema Manase.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani Geita Mponjoli
Mwabulambo alipotafutwa kwa njia ya simu amesema hayupo ofisini kwa
muda huo na yupo kwenye oparesheni na anatarajia kufika jioni ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment