Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba haijapiga
marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu badala yake
walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita kujiunga na
vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.
Aidha, imesema kwa
waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa waajiri wao
kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa hiyo kufanya
mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu Waziri wa wizara
hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na
taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku
watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye
sifa za kidato cha sita.
Manyanya alisema kwa
waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za shahada kwa
kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo waliyofeli na
kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa
ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni vitu
tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu anakaa nafasi kwa
sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki utafanyika kwa vyeti na wanaofanya
hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu Waziri.
Alisema kwa
watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa
wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia
njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa
taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa siku
ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli kuingia kwenye
‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna
kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza
Manyanya akirejea kauli ya Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni
katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako
alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami ningependa
nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa. Kama sifa ya
kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama amefeli Baraza la
Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini
tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza Waziri Ndalichako.
Naibu Waziri alisema
kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa moja na njia ya
mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika
ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.
“Tanzania imejiwekea
mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa katika utoaji wa
elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu wengi
zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua
elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema walitambua
kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu, lakini hawapati hiyo fursa
na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu Huria na mtu anaweza kusoma alipo
na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi siku.
Alisema iliwekwa
mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na hivyo siyo kila cheti
kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine na kila mamlaka imepewa
jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa nchini.
Naibu Waziri alisema
kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali kumejitokeza changamoto na watu
kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na kujiwekea mifumo binafsi ambayo
imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha nne ambao hawana sifa kuingia vyuo
vikuu.
“Jambo hilo
limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli kidato cha nne bila
kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika kozi hiyo halafu anaingizwa
chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo wa ‘foundation course’ na hatuna
vipimo vyake,” alieleza.
Alisema kwa kawaida
mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa usawa wa alama fulani na
kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya kuingia vyuo, lakini siyo waliofeli
hivyo wanatakiwa kufanya utafiti zaidi katika kozi hiyo.
“Haiwezekani kila mtu akajianzishia
mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo si zuri kama nchi na sasa tutaimarisha
ubora…ukifeli kidato cha nne unatakiwa kwenda kusoma na kupata cheti kwenye
mtaala unaotambulika na ukaenda diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo
kikuu,” aliongeza.
Naye Naibu Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema suala la ‘Foundation course’
limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu
ili kuingia chuo kikuu, lakini walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua
waliofeli kidato cha nne na sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye
kuwaingiza chuo kikuu.
No comments:
Post a Comment