Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri Serikali kuanzisha mfumo maalum wa
uwekezaji ili fedha zitakazowekwa katika mfuko huo zitumike kama mtaji katika
maeneo ambayo nchi inataka kuwekeza.
Ushauri huo umetolewa
mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka alipokuwa
akiwasilisha maoni ya kamati hiyo iliyochambuliwa kwa kina juu ya changamoto,
maombi na mapendekezo yatakayoiwezesha nchi kusonga mbele.
Mwenyekiti Mhe.
Kaboyoka amesema kuwa ushauri huo umetolewa baada ya kukwama kwa baadhi ya
miradi pamoja na shughuli nyingine za Serikali zinazofanywa ili kuwasaidia
wananchi kutokana na ukosefu wa fedha za kufanyia shughuli hizo hivyo
kuanzishwa kwa mfuko huo kutahakikisha faida ya uwekezaji inaonekana.
“Sisi kama kamati
tunaishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum wa uwekezaji kwani utaisaidia
Serikali kupata fedha za kufanyia maendeleo na kupata mitaji ya kuwekeza sehemu
mbalimbali ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa na watanzania wanaiona
faida ya uwekezaji”, alisema Mhe. Kaboyoka.
Mhe. Kaboyoka
aliongeza kuwa kamati hiyo imependekeza kuwa mfuko huo uanzishwe chini ya Ofisi
ya Msajili wa Hazina kwa kutumia mfumo wa kubakisha mapato kwa sababu ofisi
hiyo ndiyo ina mamlaka ya kugawa fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi
mbalimbali.
Aidha, taarifa ya
Mkaguzi Mkuu wa Serikali imebaini kuwa pamoja na kuwa Idara ya Uhamiaji imeweka
usimamizi wa utoaji wa viza katika Makao Makuu ya Idara, kwenye Balozi pamoja
na maeneo ya mipaka ya nchi lakini mfumo wa kutoa viza kwa wageni wanaowasili
nchini hauna mawasiliano mazuri.
Kukosekana kwa
mawasiliano hayo kunasababisha mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali
yanayotakiwa kukusanywa kutokana na utoaji wa viza hivyo kamati pia imeiomba
Serikali kukamilisha haraka mradi wa Uhamiaji Mtandao (E- Migration) ili
kuboresha njia za ukusanyaji wa mapato katika Idara hiyo.
Kwa upande wa Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyowasilishwa Bungeni hapo na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vedasto Ngombale Mwiru ambaye ameelezea matatizo
sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma katika Serikali za Mitaa pamoja na
ushauri wa kamati hiyo katika kuhakikisha tatizo hilo linakoma.
Mhe. Ngombale Mwiru
ameeleza kuwa Kamati imebaini udhaifu wa watendaji wa Halmashauri mbalimbali
nchini katika usimamizi wa mikataba ya utekelezaji wa maendeleo unaopelekea
miradi hiyo kuchelewa kukamilika, kukamilika kwa kiwango cha chini au
kutokukamilika kabisa.
“Kulingana na taarifa
hiyo, kamati imezishauri Halmashauri zote nchini kutofanya kazi kwa mazoea na
badala yake kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu ili iweze kukamilika kwa wakati
na kutumika kama ilivyo kusudiwa”, alisema Mhe.Ngombale Mwiru.
Ameongeza kuwa
kumekuwa na tatizo katika Halmashauri hizo la kutotenga asilimia 10 ya fedha za
mapato kutoka katika vyanzo vya ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana
ambapo kuna baadhi ya Halmashauri hazijawasilisha michango hiyo kwa zaidi ya
miaka mitatu.
Kutokana na tatizo
hilo, Kamati imetoa agizo kwa Halmashauri zote kuandika barua ya kuthibitisha
kulipa madeni hayo pia kuelezea mipango watakayotumia katika kutekeleza ulipaji
huo.
Pia Kamati imeishauri
Serikali kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya wanawake na
vijana ili iwe sheria ambayo itatekelezwa kwa lazima hivyo kuendelea kuinua
maisha ya wanawake na vijana kama ilivyokusudiwa.
Baada ya kamati zote
mbili kuwasilisha taarifa hizo mbele ya Bunge,sasa ni zamu ya wabunge kujadili
kwa kina masuala yaliyozungumziwa katika taarifa hizo kwa kutoa maoni yao na
kuishauri Serikali kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika matumizi ya fedha kwa
kuyapatia ufumbuzi ili yasijirudie katika taarifa zijazo.
No comments:
Post a Comment