Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa uboreshaji huduma za Umeme
Serikali imedhamiria
kuimarisha mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme nchini ili kufikia
malengo ya Taifa ya Asilimia 75 ya watanzania wanaonufaika na huduma ya umeme
ifikapo 2025.
Hayo yamesemwa leo
jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa Uzinduzi wa
Mradi wa uboreshaji huduma za Umeme Jijini Dar es Salaam wenye lengo la
kuboresha usambazaji na usafirishaji wa umeme katika jiji hilo.
Mhe. Majaliwa alisema
kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imekuwa katika jitihada
mbalimbali za kuboresha miundombinu yake ili hatimaye huduma hiyo ili iweze
kuwafikia wananchi wengi na katika ubora unaohitajika.
“Nimeambiwa kuwa mradi
huu wa kuboresha miundombinu ya umeme ulilenga kuimarisha upatikanaji wa huduma
ya umeme wa uhakika hususani katika jiji la Dar es Salaam, hivyo kukamilika kwa
mradi huu kutafungua fursa nyingi za uzalishaji na kupelekea upatikanaji wa
fursa za ajira za uhakika kwa wananchi” alifafanua Waziri Mkuu.
Mhe. Majaliwa alisema
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza ahadi yake ya kusambaza
na kuwapatia wananchi umeme wa uhakika ili kuweza kufanikisha shughuli za
kiuchumi kwa ufanisi na hivyo kuongeza pato la Taifa.
“Serikali inayoongozwa
na Chama cha Mapinduzi iliahidi kuendeleza kusambaza umeme wenye uhakika Mijini
na Vijijini, hivyo Serikali imara inayojali maslahi ya wananchi wake ni ile
inayotoa ahadi na kuzitekeleza” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu
alisema kuwa upatikanaji wa Umeme wa uhakika utaiwezesha nchi kufikia uchumi wa
kati kupitia viwanda ikiwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa upande wake Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameutaka uongozi wa TANESCO
kushughulikia na kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme nchini kwani kufikia
uchumi wa kati kupitia viwanda itahitaji umeme wa uhakika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi.
Felchesmi Mramba alisema kuwa Mradi huo umetumia jumla ya Shilingi bilioni
74.6, ikiwa ni fedha kutoka Serikali ya Finland kwa kushirikiana na
Serikali ya Tanzania.
Mhandisi. Mramba aliongeza kuwa Mradi huo utasaidia
kuvutia wawekezaji wapya katika Sekta za viwanda na biashara nchini.
Pia Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland Bw. Kai
Mykkanen, alisema kuwa Serikali ya Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania
katika masuala ya maendeleo hususani katika sekta ya Nishati.
No comments:
Post a Comment