Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome
Serikali imezitaka
taasisi zinazosimamia mtandao wa haki za binadamu katika nchi za Afrika
Mashariki kupanua wigo wa utoaji elimu kwa umma, hatua inayolenga kutatua
migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza katika jamii.
Wito huo umetolewa leo
Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
Prof. Sifuni Mchome, wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa
taasisi zinazosimamia Haki za Binadamu katika nchi za Afrika Mashariki.
Prof. Mchome alisema
jukumu la ulinzi na usimamizi wa haki za binadamu katika eneo la jumuiya hiyo
ni la kila nchi mwanachama, kwa kuwa msingi wa maendeleo wa nchi yoyote duniani
hupatikana katika sehemu yenye hali ya utulivu na maeleweno.
Kwa mujibu wa Prof.
Mchome alisema kuanzia mwezi Mei hadi Septemba mwaka huu, nchi zote za Afika
Mashariki ziliwasilisha taarifa zao kuhusu hali ya haki ya kibinadamu katika
mataifa yao, mjini Gevena Uswisi, ambapo ripoti hizo zitatumika katika kujadili
changamoto zilizojitokeza na hatua za kuchuliwa katika kuboresha.
Aidha Prof. Mchome
alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika kuimarisha
haki za kibinadamu duniani ingawa yapo maeneo kadhaa yenye migogoro
ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji, ingawa Serikali imechukua hatua za
makusudi za kukabiliana na hali hiyo.
“Serikali imekuwa
ikipeleka taarifa Bungeni kuhusu migogoro ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji, na maamuzi ya kisera yanayofanywa na Serikali, pamoja na kuendelea
kuelimisha umma kuhusu masuala ya sheria mkononi.” Alisema Prof. Mchome.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAG), Mary Massay
alisema suala la haki za binadamu ni dhana mtambuka kwa kuwa inagusa sekta
muhimu za maisha ya binadamu ikiwemo elimu, maji, ardhi, maliasili na
kadhalika.
Alisema mkutano huo
umeandaliwa makhususi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya ripoti za
utafiti kuhusu hali ya haki za binadamu katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo
Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.
Alisema utafiti huo
umejikita zaidi katika kubaini viashiriia vya uvunjifu wa haki za baindamu
katika nchi hizo na hatua zinazopaswa kuchuliwa na Serikali za nchi wanachama
ili kuzuia machafuko katika siku za usoni kutokana uzoefu uliojitokeza
katika nchi za Rwanda na Burundi.
Kwa mujibu wa Massay
alisema migogoro mingi inayotokeza katika nchi nyingi za Afrika hususani
zilizopo katika ukanda wa Afrika mashariki husababishwa na kauli na matamko ya
viongozi kuagiza jambo ambalo linakwenda kinyume na matakwa ya wananchi walio
wengi.
Naye Naibu Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu ya nchini Kenya, George Morara alisema hali ya haki
za kibinadamu ya nchi hiyo ni ya kurithisha ingawa mamlaka za dola katika nchi
hiyo zimekuwa zikikuwa zikitumia nguvu kubwa kuthibiti raia kwa kutumia sheria zilizopo.
Alisema
miongoni mwa sheria ni sheria ya kimataifa inayohusu haki za kiraia na kisiasa
ambapo, baadhi ya maafisa usalama nchini humo wamekuwa wakitumia nguvu kuzuia
mikusanyiko ya kisiasa kwa kigezo cha kudhibiti matukio ya kigaidi nchini humo.
No comments:
Post a Comment