Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Prof Jumanne Maghembe akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika
kikao cha tisa cha mkutano wa tano wa Bunge la 11linaloendelea Mjini Dodoma
Novemba 10, 2016.
Serikali imejipanga
kuboresha miundo mbinu ya Chuo cha Misitu cha Olmotonyi kilichopo katika Jimbo
la Chambani Mkoa wa Kusini Pemba ili kuwavutia wanafunzi kujiunga na chuo hicho
hivyo kuongeza idadi ya wataalamu wa misitu nchini.
Hayo yamesemwa leo
mjini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chambani Mhe. Yussuf Hussein lililohoji
juu ya mpango wa Serikali kukiboresha chuo hicho.
Prof. Maghembe amesema
kuwa wameamua kuboresha miundo mbinu ya chuo hicho kwa sababu kumekuwa na
upungufu mkubwa wa wataalamu wa misitu nchini ambapo kwa sasa kila mtaalamu wa
misitu anasimamia jumla ya hekta 25,000 za misitu kinyume na uwiano
unaokubalika kimataifa wa mtaalamu mmoja kusimamia hekta 5000.
”Serikali
yetu kwa kushirikiana na Serikali ya Norway inaendelea kutekeleza mradi wa
Kuwezesha Jamii kupitia Mafunzo ya Shughuli za Usimamizi Shirikishi wa Misitu
pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi, mradi ambao tuna uhakika utakijengea chuo
uwezo na kukiboresha zaidi”, alisema Mhe. Maghembe.
Mhe. Maghembe
ameyataja malengo ya mradi huo kuwa ni kukarabati nyumba saba za watumishi,
kuimarisha maktaba ya chuo kwa kuweka samani, vitabu 137 vya mada 22 tofauti,
kuweka vifaa 62 vya kufundishia, kompyuta 15 na kutoa mafunzo ya kompyuta kwa
wakutubi watano, ukarabati wa mtandao wa mawasiliano pamoja na kuunganisha Chuo
na mkongo wa Mawasiliano wa Taifa.
Mhe. Prof Maghembe
ameongeza kuwa mradi huo unaendelea na ujenzi wa bweni moja lenye uwezo wa
kuchukua wanachuo 100 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo
200 kwa wakati mmoja.
Aidha, mradi huu
utawajengea uwezo wa mbinu bora za kufundishia wakufunzi 16 na kutoa mafunzo
kwa jamii za vijijini kuhusu kuhifadhi misitu na shughuli mbadala za kiuchumi.
Mhe. Maghembe
amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kutoka mwaka 2013
hadi 2016 Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
imegharamia ukarabati wa nyumba 9 za watumishi, kumbi za chakula kugharamia
mikutano na ununuzi wa kompyuta mbili na gari aina ya Tata kwa ajili ya usafiri
kwa mafunzo ya vitendo nje ya Chuo pia kupitia mradi huo Serikali inatoa
ufadhili kwa wanafunzi wa ngazi ya Astashahada na Stashahada.
No comments:
Post a Comment