Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha akijibu hoja
mbalimbali za wabunge katika Bunge la 11 Mjini Dodoma.
Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhamishia Bodi ya Pamba katika Mkoa wa Mwanza kabla
ya Novemba 10 mwaka huu ili kuhakikisha wakulima wa pamba waliopo katika mkoa
huo wanapata huduma zilizo bora kwa ukaribu na haraka.
Hayo yamesemwa leo
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. William Ole Nasha
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bukombe Mhe. Doto Biteko lililohoji juu ya
hatua ya Serikali kwa wakulima walioathirika na pembejeo zilizotolewa ambazo
hazikuwa na ubora pamoja na kuhamishia Bodi ya Pamba katika mkoa huo.
”ili kuwafikia
kirahisi wakulima wa pamba waliopo mkoani Mwanza, Wizara imeamua kuhamishia
Bodi hiyo katika mkoa huo na kwa taarifa zilizopo Bodi hiyo inatakiwa kuhama
haraka iwezekanavyo kabla ya Novemba 10 mwaka huu”, alisema Mhe.Ole Nasha.
Kwa upande wa matatizo
ya pembejeo, Mhe. Ole Nasha amesema kuwa Serikali tayari ina taarifa kuhusu
tatizo lililowapata wakulima wa pamba katika maeneo mbalimbali kwa kusambaziwa
viuatilifu pamoja na mbegu ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa hivyo kuathiri wakulima
nchini.
“Serikali iliiagiza
Tropical Pesticides Research Institute (TPRI) kufanya uchunguzi wa malalamiko
ya wakulima ambao ulibaini kuwa viuatilifu hivyo vilikuwa na utendaji hafifu
hivyo Serikali itaanza kuzalisha mbegu bora za pamba za UK08 ili kuhakikisha
tatizo hili halijirudii tena”, alisema Mhe. Ole Nasha.
Naibu Waziri huyo
amefafanua kuwa kufuatia changamoto hizo za uotaji wa mbegu, Serikali iliamua
kufanya majaribio ya utoaji wa mbegu ambazo zilikuwa zikisambazwa hapo awali
bila kujua ufanisi katika uotaji wake.
Amethibitisha kuwa,
matokeo ya jaribio hilo yamewezesha kutoa maelekezo kuhusu aina za mbegu za
pamba zenye sifa za msingi ambazo zitasambazwa kwa wakulima katika msimu wa
kilimo wa mwaka 2016/2017.
No comments:
Post a Comment