Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo
cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe.
Samwel Sitta.
Mhe. Samwel Sitta
amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University
of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika salamu hizo,
Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za
kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa
mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee
Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli
katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na
Serikali.
“Kupitia kwako Mhe.
Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote
walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema
anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na
amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi
Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
No comments:
Post a Comment